ZIARA YA WAZIRI MKUU MUSOMA VIJIJINI: SERIKALI KUENDELEA KUJENGA KWA KIWANGO CHA LAMI BARABARA LA MUSOMA-MAKOJO-BUSEKERA (km 92)

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Kassim Majaliwa Majaliwa amewaeleza wana-Musoma Vijijini kuhusu uamuzi wa Serikali kuendelea kutoa fedha nyingi za utekelezaji wa miradi ya maendeleo vijijini mwao.

Waziri Mkuu aliyasema hayo kwenye mkutano wake wa hadhara uliofanyika Kijijini Bwai Kwitururu, Musoma Vijijini siku ya Alhamisi, tarehe 29.2.2024

Barabara kuendelea kuwekewa lami:
Serikali imesema itaendelea kulijenga barabara letu kuu na muhimu la Musoma-Makojo-Busekera lenye urefu wa kilomita 92 kwa kiwango cha lami. Tuzingatie yafuatayo kutoka Serikalini:

(i) Kilomita 5 zimeishawekewa lami
(ii) Barabara limo kwenye Bajeti ya mwaka huu (2023/2024)
(iii) Kibali kimetolewa barabara litangazwe na Mkandarasi apatikane, na aendelee na ujenzi.

Tafadhali sikiliza kwa makini hadi mwisho CLIP/VIDEO iliyoambatanishwa hapa, hasa penye kauli ya Serikali kuhusu barabara la Musoma-Makojo-Busekera.

Shukrani:
Wana-Musoma Vijijini tunaendelea kuishukuru Serikali yetu, chini ya uongozi mzuri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha nyingi za kufadhili miradi ya maendeleo vijijini mwetu.

Tunamshukuru sana Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Tanzania, Mhe Kassim Majaliwa Majaliwa kwa kututembelea Jimboni mwetu, na kwa kuendelea kufuatilia utekelezaji wa miradi yetu ya maendeleo ambayo ni kielelezo cha mafanikio ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2020-2025.

Ofisi ya Mbunge
Jimbo la Musoma Vijijini
www.musomavijijini.or.tz

Tarehe:
Jumatatu, 4.3.2024