Mbunge

Prof. Sospeter Muhongo

Prof. Sospeter Muhongo

Prof. Sospeter Muhongo, Mbunge wa Musoma Vijijini, ni mwanazuoni maarufu na pia mwanajiolojia mbobevu.

Prof Muhongo aliongoza na kusimamami mabadiliko endelevu ya ubunifu na ugunduzi katika Sekta za Nishati na Madini nchini mwetu kwa kuingiza sera mpya na kutengeneza nyaraka za kisheria. Pia ameongeza idadi ya rasilimali watu iliyopata mafunzo mazuri ya kitaaluma katika Tasnia ya Mafuta na Gesi Asilia. Amesimamia ongezeko la kasi kubwa ya kampeni ya usambazaji umeme vijijini, na amesimamia usambazaji wa haraka na wa uhakika wa umeme mijini. Amesimamia punguzo kubwa la gharama za kuunganishiwa umeme vijijini na mijini. Amesimamia ongezeko la mapato katika Serikali Kuu na Serikali za Mitaa kutokana na kodi na tozo mbalimbali kwenye madini yetu.

Prof Muhongo amevutia uwekezaji mpya (kutoka ndani na nje ya nchi) wenye mitaji midogo na mikubwa kwenye Sekta za Nishati, Madini, Mafuta na Gesi Asilia. Haya yote yamechangia ukuaji mzuri wa uchumi wetu.

Prof Muhongo na watafiti wenzake wamechapisha ramani kwa kuzingatia dhana na maarifa ya kisasa ya Jiolojia, kama vile: Jiolojia na Mashapo Makubwa ya Madini ya Afrika, Jiolojia na Mashapo ya Vito vya Thamani vya Afrika Mashariki na Ramani ya Jiolojia na Madini ya Tanzania. Hakuna mikopo au misaada ya fedha ilitumika kutengeneza ramani hizi. Ramani hizi zinatumika kupanua na kukuza uwekezaji mpya katika Sekta ya Madini Barani Afrika.

Kama Mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini, anavyo vipaumbele vyake kwa ajili ya kuleta maendeleo ya wananchi na jimbo kwa ujumla. Vipaumbele hivi ni pamoja na: Elimu bora kwa wote, Huduma bora za Afya kwa wote, Kilimo cha Kisasa kwa mazao ya biashara na chakula, Kuongeza ajira, na Kupatikana kwa maji safi na salama kwa wananchi wote.

Mheshimiwa Muhongo ni Profesa Kamili (mstaafu) wa Jiolojia katika Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam na Profesa wa Heshima wa Jiolojia katika Chuo Kikuu cha Pretoria, Afrika Kusini. Ni mjumbe wa bodi kadhaa za uhariri wa majarida ya sayansi na vijarida vya sayansi, teknolojia na ubunifu. Yeye ni Mhariri Mwandamizi wa Kitabu cha Mwaka 2009 kiitwacho: Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kwa Maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii: Simulizi za Mafanikio kutoka Afrika (“Science, Technology and Innovation for Socio-Economic Development: Success Stories from Africa”). Alisomea Jiolojia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Tanzania) na Gӧttingen (Ujerumani). Alihitimu na kutunukiwa shahada ya Dr.rer.nat. kutoka Technical University of Berlin, Ujerumani. Prof. Muhongo anaongea, na kuandika kwa ufasaha na umahiri mkubwa Kiswahili, Kiingereza na Kijerumani, na kwa wastani kwa lugha ya Kifaransa.