WANAKIJIJI WANAJENGA MAKTABA, VYUMBA VIPYA VYA MADARASA NA OFISI YA WALIMU KWA WAKATI MMOJA

WANAVIJIJI wakiwa kwenye ujenzi wa MAKTABA ya S/M BUTATA, Kijijini Butata. Kata ya Bukima. Ujenzi huo umepangwa kukamilika kabla ya tarehe 15 Juni 2020.

USHIRIKIANO MZURI kati ya WANANCHI, SERIKALI, VIONGOZI wa Kata na Kijiji, na WADAU wa MAENDELEO unazaa matunda mazuri kwenye ujenzi na uboreshaji wa MIUNDOMBINU ya ELIMU kwenye Kijiji cha Butata, Kata ya Bukima.
WANAKIJIJI wa Kijiji cha Butata wanachangia NGUVUKAZI (kusomba mchanga, mawe, kokoto na maji) na Tsh 4,000 (elfu nne) kutoka kila KAYA kwenye ujenzi wa MAKTABA, VYUMBA 2 VIPYA vya MADARASA na OFISI 1 ya WALIMU ya S/M BUTATA. DIWANI wao, Mhe January Simula amechangia Saruji Mifuko 5. Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji, Ndugu William Kugosora – HONGERENI SANA WANA-BUTATA!
Leo, Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof Sospeter Muhongo amechanga SARUJI MIFUKO 50 na kukamilisha AHADI yake ya SARUJI MIFUKO 100 kwa ajili ya ujenzi unaondelea Shuleni hapo.
Baada ya kukamilika kwa MAKTABA ya Shule hiyo, Mbunge huyo ataiongezea Shule hiyo VITABU vingine vya MAKTABA.
Leo, PCI (Plan Concern International),  IMETHIBITISHA AHADI yake ya kukamilisha ujenzi wa MAKTABA hiyo kama ifuatavyo: kuezeka jengo, kukamilisha jengo ndani na nje (finishing) na kuweka samani za maktaba – AHSANTE SANA PCI!
WADAU wengine wa MAENDELEO wanaochangia UJENZI kwenye Shule hiyo ni: Ndugu Samson Masawa (USA) na Ndugu Muya Essero – hawa ni WAZALIWA wa Kijiji cha Butata  – AHSANTENI SANA!
MWALIMU MKUU wa Shule hiyo,  Mwl Yohani Dawi amesema kwamba FEDHA zitokazo SERIKALINI kwa ajili ya ukarabati wa MIUNDOMBINU zimechangia sana ujenzi huu. Vilevile, HALMASHAURI yetu inakusudia kuchangia ujenzi huu  – AHSANTE SANA SERIKALI na HALMASHAURI yetu!
DIWANI wa Kata ya Bukima yenye VIJIJI 3 vya Butata, Kastamu na Bukima, Mhe January Simula ANAWASHUKURU sana WANANCHI wa Kijiji cha Butata kwa kupata ARI MPYA ya kukamilisha MIRADI ya ujenzi wa MAKTABA, VYUMBA vipya vya Madarasa, OFISI ya Walimu, ZAHANATI, OFISI ya Kijiji na Shule MPYA ya Msingi.
DIWANI huyo ameishukuru sana SERIKALI na HALMASHAURI yetu kwa kuendelea kuchangia UBORESHAJI wa MIUNDOMBINU ya ELIMU kwenye Kata ya Bukima.
WADAU wengine wa Maendeleo kwenye SEKTA ya ELIMU ndani ya Kata hiyo ni: PCI, USA (vitabu, ujenzi wa vyoo, matenki ya maji, kilimo cha chakula cha wanafunzi,  na mafunzo mbalimbali), BMZ, Ujerumani (vifaa vya elimu kwa wanafunzi wenye ulemavu), na baadhi ya WAZALIWA wa Kata ya Bukima.
MBUNGE wa JIMBO, Prof Sospeter Muhongo ametoa MICHANGO mingi kwenye SEKTA ya ELIMU ndani ya Kata hiyo ikiwemo ya: (i) Madawati kwa Shule zote za Msingi, (ii) Vitabu vya Maktaba kwa Shule zote za Msingi na Sekondari (iii) Saruji na Mabati.
MFUKO wa JIMBO nao umechangia Saruji na Mabati kwenye Sekta ya Elimu ndani ya Kata ya Bukima.
KARIBUNI TUCHANGIE UJENZI na UBORESHAJI wa MIUNDOMBINU YA ELIMU KWENYE KATA YA BUKIMA