WALEMAVU KWIKUBA GROUP WAPOKEA MKOPO USIOKUWA NA RIBA KUTOKA HALMASHAURI YAO

Baadhi ya Wana-Kikundi cha WALEMAVU KWIKUBA GROUP wakiwa kwenye MRADI wao wa UFUGAJI wa KONDOO na MBUZI, Kijijini Kwikuba, Kata ya Busambara.

Na: Hamisa Gamba
Msaidizi wa Mbunge
KIKUNDI cha Watu wenye ULEMAVU kiitwacho, “WALEMAVU KWIKUBA GROUP” kilianzishwa Februari 2019 kikiwa na WANACHAMA 26 ambao kwa sasa wamefika 41.
WALEMAVU KWIKUBA GROUP yenye maskani yake Kijijini Kwikuba, Kata ya Busambara ilianza kwa KUUZA NAFAKA na wamepanua biashara yao na kuanza KUFUGA KONDOO na MBUZI baada ya kupata MKOPO usiokuwa na RIBA wa Tsh 2,400,000 kutoka HALMASHAURI ya Wilaya ya Musoma yenye Jimbo la Musoma Vijijini.
MWENYEKITI wa Kikundi hiki, Ndugu John Ndaro Musulubhi alisema kuwa Kikundi chao KIMESAJILIWA na HALMASHAURI yao na LENGO lao kuu ni KUJITEGEMEA KIUCHUMI kutokana na MAPATO ya BIASHARA zao za NAFAKA na MIFUGO.
MWENYEKITI huyo anaishukuru sana HALMASHAURI ya Wilaya ya Musoma na VIONGOZI wake kwa kutoa MIKOPO isiyokuwa na RIBA kwa WATU wenye ULEMAVU walioko ndani ya Halmashauri hiyo.
MBUNGE wa Jimbo, Prof Sospeter Muhongo ametunisha MTAJI wao wa biashara ya NAFAKA kwa kuwanunulia MAGUNIA KUMI (10) ya MAHINDI na amesema watawasaidia kutafuta WADAU wengine wa Maendeleo watakaowatunishia MTAJI wao wa biashara.
Sambamba na MAFANIKIO hayo, WALEMAVU KWIKUBA GROUP  wanataraji kuanzisha  MRADI wa USEREMALA, na wanaomba WADAU wa MAENDELEO na hasa kwa WATU wenye ULEMAVU, wajitokeze kuwasaidia wapate VIFAA VYA USEREMALA.
WALEMAVU KWIKUBA GROUP wanawashauri na kuwashawishi WATU WENYE ULEMAVU po pote walipo kutumia FURSA zinazotolewa na SERIKALI yetu ya kuwafanya WAJITEGEMEE KIUCHUMI.