WATOTO WADOGO WA KIJIJI CHA BURAGA KUEPUKA KUTEMBEA KILOMITA 4-5 KWENDA MASOMONI

Washiriki wa KIKAO cha leo cha WAKAZI wa Kitongoji cha Mwaloni, Kijijini Buraga, na Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof Sospeter Muhongo.

KIJIJI CHA BURAGA, Kata ya Bukumi kina VITONGOJI 6 ambavyo vinahudumiwa na SHULE MOJA YA MSINGI (S/M Buraga) iliyo kwenye Kitongoji cha Musokwa.
WATOTO wenye umri kati ya miaka 6 na 15 wa KITONGOJI cha MWALONI wanalazamika kutembea umbali wa kilomita 4-5 kwenda MASOMONI kwenye S/M BURAGA.
WAKAZI wa KITONGOJI cha MWALONI wameamua kuanzisha SHULE YA AWALI chini ya MTI ndani ya Kitongoji hicho. Wakati huo huo WAKAZI hao hao WAMEAMUA KUJENGA SHULE SHIKIZI karibu na Darasa hilo la chini ya MTI.
Leo, Jumanne, 10 March 2020, Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof Sospeter Muhongo amefanya ZIARA KIJIJINI BURAGA kukagua MIRADI YA MAENDELEO ukiwemo MRADI WA UJENZI WA SHULE SHIKIZI YA BURAGA MWALONI.
Ndugu Nyajoge Chirya, Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi ametoa RIPOTI ya ujenzi wa Shule Shikizi hiyo na kusema ifikapo tarehe 15 March 2020, UJENZI uliosimama kwa muda, utaendelea kwa KASI KUBWA zaidi.
MICHANGO YA UJENZI WA SHULE SHIKIZI BURAGA MWALONI
* NGUVUKAZI na FEDHA Taslimu vinachangwa na Wakazi wa Kitongoji cha Mwaloni.
* MDAU wa Maendeleo, rafiki ya Mbunge wa Jimbo (Prof Sospeter Muhongo) alichangia SARUJI MIFUKO 5.
* MFUKO wa Jimbo la Musoma Vijijini umeishachangia SARUJI MIFUKO 50
* Mbunge wa Jimbo, Prof Sospeter Muhongo atachangia SARUJI MIFUKO 100 kuanzia tarehe 15 March 2020 (ujenzi uliosimama utakapoendelea).
SHULE SHIKIZI HIYO itafunguliwa rasmi Januari 2021. Huo ndio UAMUZI wa Wakazi wa Kitongoji cha Mwaloni, Kijijini Buraga.
OMBI KUTOKA KWA WANANCHI WA KIJIJI CHA BURAGA, KATA YA BUKUMI
* Wananchi wa Kijiji cha Buraga wanaomba WAZALIWA WA KIJIJI hicho na Kata ya Bukumi kwa ujumla WAANZE KUCHANGIA MIRADI ya MAENDELEO ya nyumbani kwao.
JIMBO la Musoma Vijijini lina Jumla ya Vitongoji 374 na Vijiji 68. JIMBO hili lina Jumla ya SHULE za MSINGI 111 za Serikali na 3 za Binafsi. SHULE SHIKIZI 11 zinajengwa na nyingine tayari zimefunguliwa.