WANAVIJIJI WAAMUA SEKONDARI MPYA INAYOJENGWA IWE NA MIUNDOMBINU YA AWALI IFIKAPO TAREHE 1 MEI 2020

KIKAO cha Jumatatu, 9 March 2020 cha WANAVIJIJI na Mbunge wa Jimbo, Prof Sospeter Muhongo wakiwa kwenye eneo la ujenzi wa Seka Secondary School.

WANAVIJIJI wa Kata ya Nyamrandirira WAMEAMUA ujenzi wa SEKONDARI MPYA ya KATA yao iwe na MIUNDOMBINU ya kuchukua WANAFUNZI wa Kidato cha Kwanza ifikapo tarehe 1 Mai 2020.
KATA ya NYAMRANDIRIRA ina Vijiji vitano (5) ambavyo ni Chumwi, Kaboni, Kasoma, Mikuyu na Seka. Vijiji vyote 5 vinahudumiwa na Sekondari moja (Kasoma Secondary School) ambayo chimbuko lake ni Kasoma Middle School iliyojengwa Mwaka 1956.
WANAFUNZI 204 wa Kidato cha Kwanza (2020) wa Kasoma Sekondari WAMERUNDIKANA ndani ya Vyumba 2 vya Madarasa. Maoteo ya Mwakani (2021) ni kuwa na WANAFUNZI 318 wa Kidato cha Kwanza kutoka Vijiji vitano (5) hivyo na vitahitajika Vyumba   8 vya Madarasa.
MIRUNDIKANO MADARASANI NA UMBALI MREFU
Mbali ya MIRUNDIKANO madarasani bado lipo tatizo la umbali mrefu wa kutembea kwa baadhi ya WANAFUNZI na WALIMU. Kwa hiyo, SULUHISHO ni KUJENGA Sekondari ya pili ndani ya Kata hiyo.
SEKA SECONDARY SCHOOL
UAMUZI ulifanywa na WANANCHI wa Vijiji 5 vyote kwamba SEKONDARI MPYA ijengwe Kijijini Seka na iitwe Seka Secondary School.
IFIKAPO TAREHE 1 MAI 2020 Sekondari Mpya hiyo inayojengwa Kijijini Seka itakuwa na MIUNDOMBINU ifuatayo: (i) Vyumba vipya 8 vya Madarasa, (ii) Vyoo matundu 10, yaani 4 ya Wasichana, 4 ya Wavulana na 2 ya Walimu. Ujenzi utaendelea wa Maabara, Jengo la Utawala, Nyumba za Walimu, Vyumba vya Madarasa na Vyoo vingine zaidi.
MICHANGO YA UJENZI
* WANAVIJIJI wanachangia NGUVUKAZI na FEDHA TASLIMU
* WADAU wakiwemo Wawekezaji wameombwa waanze kuchangia
* Mbunge wa Jimbo, Prof Sospeter Muhongo ameanza kuchangia SARUJI MIFUKO 250 (kila Kijiji kupewa Mifuko 50).
* WAZALIWA wa Kata ya Nyamrandirira na RAFIKI zao WANAOMBWA waanze kuchangia ujenzi huu.
JIMBO la Musoma Vijijini lina Kata 21 na Vijiji 68. Jimbo hili lina Jumla ya Sekondari 20 za Kata/Serikali na 2 za Binafsi. Sekondari Mpya 5 zinajengwa kwa MALENGO ya kufunguliwa Mwakani (Januari 2021).