WANAVIJIJI WADHAMIRIA KUACHANA NA JEMBE LA MKONO

baadhi ya Wanachama wa KIKUNDI cha KILIMO cha Kijijini Butata, Kata ya Bukima, kiitwacho, “FUKUZA NJAA”, kikiwa kazini kikitumia PLAU badala ya JEMBE la MKONO.

Na: Veredian Mgoma
Msaidizi wa Mbunge
VIKUNDI VYA KILIMO 20 kutoka VIJIJI 20 vimeanza kurahisisha KILIMO chao kwa kutumia PLAU (jembe linalokokotwa na ng’ombe) badala ya kutumia JEMBE LA MKONO.
Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof Sospeter Muhongo alitoa ZAWADI YA MWAKA MPYA (2020) ya PLAU 20 kwa VIKUNDI hivyo 20.
Ndugu Makuke Mnubi ni Mkulima wa Kijiji cha Chimati, Kata ya Makojo ambae KIKUNDI chake kilipewa zawadi ya PLAU moja. Kwa muda mfupi sana na bila kutumia nguvu nyingi waliweza kulima EKARI 6 kwa kutumia PLAU hiyo na wamepanda MPUNGA  na   MAHINDI.
Ndugu George Tole ni mkulima wa Kijiji cha Butata, Kata ya Bukima na yuko kwenye KIKUNDI CHA FUKUZA NJAA. Mkulima huyo amesema WANAVIJIJI wamevutiwa sana na  KILIMO cha kutumia PLAU na wengine  wameanza kutumia  PUNDA wao (mbali ya ng’ombe) kukokota PLAU yao na hadi sasa wamelima EKARI 7 za MAJARUBA ya MPUNGA na wamelima EKARI 5 nyingine ambazo wamepanda MAHINDI, MIHOGO na VIAZI LISHE.
Kwa nyakati tofauti VIONGOZI wa VIKUNDI vya KILIMO vilivyopewa PLAU, wanamshukuru sana Mbunge wao Profesa Muhongo kwa kushirikiana na WAKULIMA kuboresha SEKTA ya KILIMO Jimboni mwao.
KAMPENI YA  ZAO JIPYA LA BIASHARA NA UTUMIAJI WA PLAU
WAKULIMA wa Jimbo la Musoma Vijijini WAMEDHAMIRIA kuachana na JEMBE LA MKONO la mababu zao. VIKUNDI VYA KILIMO vinaendelea kuundwa kwa ajili ya MATUMIZI ya pamoja ya PLAU na Vikundi vingine (AMCOS) vinashawishiwa vichukue mikopo ya MATREKETA.
Mbali ya KAMPENI ya kutokomeza JEMBE la MKONO, Mbunge huyo kwa kushirikiana na MAAFISA KILIMO wanaendelea kushawishi WAKULIMA walime zao JIPYA la ALIZETI  Vijijini mwao. Kwa MISIMU 3 mfululizo Mbunge huyo AMEGAWA BURE TANI 9.7 za Mbegu za ALIZETI na Wizara ya Kilimo ilitoa bure TANI 10 za Mbegu za ALIZETI kwa WAKULIMA wa Jimbo hilo.
KILIMO CHA MIHOGO nacho kinaboreshwa Jimboni humo kwa kutumia MBEGU ya aina ya MKOMBOZI inayopendekezwa na WATAALAMU wa KILIMO. Mbunge wa Jimbo aligawa bure MAGUNIA 796 ya Mbegu ya Mkombozi kwa Wakulima wa Jimbo hilo. Vilevile, kwa kupambana na athari za tabianchi, Mbunge huyo aligawa bure TANI 7.7 za MTAMA Jimboni humo.
Kwa kuendelea kuboresha Kilimo ndani ya Jimbo la Musoma Vijijini, FEDHA za MFUKO WA JIMBO zilitumika kununua VIFAA VYA UMWAGILIAJI na MBEGU kwa VIKUNDI 15 vya Vijana na Wanawake.
VIKUNDI VYA KILIMO VYA VIJIJI 20
Vikundi 20 vilivyopewa zawadi ya PLAU vinatoka Vijiji vifuatavyo:
Bukima, Butata, Chimati, Chitare, Chumwi, Mabui Merafuru, Masinono, Mikuyu, Kaburabura, Kamguruki, Kwibara, Maneke, Mwiringo, Nyakatende, Nyasaungu, Nyegina, Rusoli, Suguti, Tegeruka na Wanyere
WAZALIWA wa Vijiji vya Jimbo hili wanaombwa kuchangia UNUNUZI WA PLAU kwa Wakulima wa Vijijini mwao.
KUTOKOMEZA UTUMIAJI MKUBWA WA JEMBE LA MKONO  INAWEZEKANA, JITOKEZE NA CHANGIA KIJIJI CHAKO!