KATA YENYE VIJIJI 4 YAAMUA KUJENGA SEKONDARI YA PILI

Viongozi wa Serikali ya Vijiji vya Kigera na Kakisheri, na baadhi ya Wananchi wakiendelea na kazi za ujenzi wa KIGERA SEKONDARI.

Jumatatu, 17.2.2020
Jimbo la Musoma Vijijini
KATA ya NYAKATENDE ina Vijiji 4, ambavyo ni: Kamguruki, Kakisheri, Kigera na Nyakatende.
NYAKATENDE SEKONDARI iliyoanzishwa Mwaka 2006 inahudumia Wanafunzi wa kutoka Kata 2 za Nyakatende (Vijiji 4)  na Ifulifu (Vijiji 3). Sekondari hii ina jumla ya WANAFUNZI 573 na WALIMU 23.
Mwalimu Mkuu wa Nyaketende Sekondari, Mwalimu Halima Selemani Yusufu amesema kwamba DARASA lenye WANAFUNZI WENGI linao 68 na lenye wachache linao 55.
Mtendaji wa Kata (WEO) Ndugu Martha Omahe Gagiri ameeleza kwamba wapo Wanafunzi wanaotembea umbali usiopungua kilomita 10 kwenda  masomoni kwenye Sekondari hiyo (kurudi nyumbani ni umbali huo huo)!
UJENZI WA SEKONDARI YA PILI
Kutokana na MATATIZO ya UMBALI na MISONGAMANO MADARASANI, Vijiji 2 vya Kigera na Kakisheri VIMEAMUA kujenga Sekondari yao kwenye Kitongoji cha Kati, Kijijini Kigera.
WAZALIWA wa Vijiji 2 hivi ambao kwa sasa wanaishi na kufanya kazi na biashara NJE ya Vijiji hivi (nje ya kwao) wameanzisha UMOJA wao wenye lengo la kusaidiana na ndugu na jamaa zao VIJIJINI kujenga SEKONDARI hii. Mwenyekiti ni Ndugu Malele Eugen Kisha na Katibu ni Ndugu Joseph Mnibhi.
HATUA NZURI IMEFIKIWA
* BOMA la Vyumba viwili (2) vya Madarasa limekamilika
* Jengo la Utawala linakaribia kukamilishwa, liko kwenye renta.
* Jengo la Maabara tatu (3) linakaribia kukamilishwa
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kigera, Ndugu Magafu Katura amesema ujenzi ulioelezwa hapo juu utakamilika kabla ya mwisho wa Mwezi huu (Februari 2020).
Mwenyekiti huyo amesema kwamba baada ya kukamilika kwa MAJENGO hayo, ujenzi unaofuata ni wa: Vyoo Matundu manne (4) ya Wasichana, manne (4) ya Wavulana na mawili (2) ya Walimu, na Nyumba ya kuishi Mwalimu Mkuu.
Diwani wa Kata ya Nyakatende, Mhe Rufumbo Rufumbo, kwa niaba ya WANANCHI wa Vijiji vya Kigera na Kakisheri ANATOA SHUKRANI nyingi kwa WADAU wote wa Maendeleo wanaochangia ujenzi wa KIGERA SEKONDARI.
MICHANGO ILIYOKWISHATOLEWA
* NGUVUKAZI za Wakazi wa Vijiji vya Kigera na Kakisheri (kusomba maji, mchanga, mawe na kokoto)
* Michango ya awali: Shilingi 2,000 kwa kila mkazi (vijiji 2) mwenye umri kati ya miaka 18 na 59.
* WAZALIWA wa Vijiji  2 wanalipa MAFUNDI na fedha nyingine zinanunua vifaa vya ujenzi.
* SARUJI MIFUKO 100 ya Mbunge wa Jimbo, Profesa Muhongo.
* SARUJI MIFUKO 100 ya Mfuko wa Jimbo
TUJIKUMBUSHE MICHANGO YA MBUNGE WA JIMBO KWA SHULE ZA MISINGI ZA VIJIJI HIVI VIWILI
S/M KIGERA
(i) Madawati 43
(ii) Vitabu vingi vya Maktaba
(iii) Saruji Mifuko 60
S/M KIGERA B
(i) Madawati 70
(ii) Vitabu vingi vya Maktaba
(iii) Saruji Mifuko 60
S/M KAMBARAGE
(Kijiji cha Kakisheri)
(i) Madawati 99
(ii) Vitabu vingi vya Maktaba
(iii) Mabati 54
(iv) Saruji Mifuko 60
(v) Saruji Mifuko 100 (Mfuko wa Jimbo)
(vi) Mbao 100 (rafiki ya Mbunge wa Jimbo)
KARIBU TUCHANGIE UJENZI WA KIGERA SEKONDARI
(Kata jirani ya IFULIFU imeanza kujenga Sekondari zake 2 kwa ajili ya Wanafunzi wa Sekondari wa Kata hiyo).