SEKONDARI MPYA ZAENDELEA KUJENGWA JIMBONI MWETU

Viongozi wa Kata na Kamati ya Ujenzi wakiwa kwenye eneo la ujenzi wa IFULIFU SECONDARY SCHOOL inayojengwa kwenye Kijiji cha Kabegi, Kata ya Ifulifu.

KATA ya IFULIFU ndiyo Kata pekee ISIYOKUWA na Sekondari yake. Kata hii yenye VIJIJI 3 (Kabegi, Kiemba na Nyasaungu) IMEAMUA kutatua tatizo hilo kwa kuanza ujenzi SEKONDARI 2 kwa wakati mmoja.
UMBALI mrefu wa kutembea, MISONGAMANO madarasani na JIOGRAFIA (k.m. Mto Nyasaungu unatenganisha vijiji hivyo) ni SABABU nilizotumiwa kufanya UAMUZI wa kuanza kujenga SEKONDARI zaidi ya moja ndani ya Kata hiyo ambayo watoto wake wanalazimika kutembea umbali mrefu kwenda Sekondari za Kata jirani za Mugango (Mugango Secondari) na Nyakatende (Nyakatende Sekondari).
Diwani wa Kata ya Ifulifu, Mhe Manyama Meru (CHADEMA) na Mtendaji Kata, Ndugu Fred Yona wamethibitisha UAMUZI wa WANANCHI wa kuamua kujenga Sekondari zaidi ya moja ndani ya Kata ya Ifulifu kwa wakati mmoja.
UJENZI WA NYASAUNGU SECONDARY SCHOOL
Hii Sekondari inajengwa na Kijiji kimoja cha Nyasaungu.
MICHANGO ya Wanakijiji wa Nyasaungu ni ya AINA YAKE kwani inategemea WINGI wa Ng’ombe alionao Mwanakijiji. Vyumba VIPYA 3 vya Madarasa vinaezekwa na Matundu 12 ya Vyoo yanachimbwa.
Mbunge wa Jimbo, Prof Sospeter Muhongo amewachangia SARUJI MIFUKO 35 na NONDO 20. Mfuko wa Jimbo umechangia MABATI 54. MIUNDOMBINU ya kuweza kuchukua Wanafunzi wa Kidato cha Kwanza itakuwa tayari kabla ya tarehe 30 Juni 2020.
UJENZI WA IFULIFU SECONDARY SCHOOL
Ujenzi umeanza hivi karibuni Kijijini Kabegi.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kabegi, Ndugu Charles Choto kwa niaba ya Kamati ya ujenzi wa Ifulifu Sekondari, alifafanua na kusema kwamba  baada ya kukamilika kwa ujenzi wa  Vyumba VIPYA viwili vya Madarasa, kazi kitakayofuata ni ujenzi wa Jengo la Utawala, Vyoo vya Wanafunzi na Walimu, Maabara na baadae nyumba ya Mwalimu Mkuu.
MICHANGO kutoka kwa Wananchi ni NGUVUKAZI na FEDHA, Shilingi 33,000/= kwa kila KAYA
HARAMBEE YA MBUNGE WA JIMBO itafanyika Jumatatu, 2 Machi 2020 kwa ajili ya KUCHANGIA ujenzi wa IFULIFU SECONDARY SCHOOL.
VIONGOZI na WANANCHI wanasema MIUNDOMBINU ya IFULIFU SekondarI ya kuweza kuchukua Wanafunzi wa Kidato cha kwanza itakuwa tayari kabla ya tarehe 30 Juni 2020.
SEKONDARI MOJA AU ZAIDI KWA KILA KATA
Hadi leo hii (9.2.2020) Jimbo la Musoma Vijijini lenye Kata 21, lina SEKONDARI 20 za Kata/Serikali, na 2 za Binafsi. Sekondari MPYA zinazojengwa na zitakuwa tayari kutumiwa ifikapo Juni 2020 ni 5 (Kigera, Nyegina, Seka, Nyasaungu na Ifulifu). MIPANGO inakamilishwa ya ujenzi wa SEKONDARI MPYA kwenye Kata 3 za Etaro, Mugango na Suguti.