KIJIJI CHA BUTATA CHAENDELEA KUTEKELEZA ILANI YA CCM – ZAHANATI MOJA KILA KIJIJI 

baadhi ya WANANCHI wa Kijiji cha Butata, Kata ya Bukima wakisomba mchanga wa ujenzi wa ZAHANATI ya Kijiji chao.

Na: Verediana Mgoma
Msaidizi wa Mbunge
Mtendaji wa Kijiji (VEO) cha Butata, Ndugu Charles Bulemo ameeleza kwamba WAKAZI wa Kijiji cha Butata wanalazimika kutembea umbali wa kilomita kati ya 3 na 6 kwenda kupata MATIBABU na HUDUMA nyingine za AFYA kwenye Zahanati ya Kijiji jirani cha Bukima.
Kata ya Bukima ina Vijiji 3 (Bukima, Butata na Kastamu). Diwani wa Kata hii, Mhe January Simula anasisitiza umuhimu wa KUTEKELEZA ILANI YA CCM (2015-2020) kwa VITENDO. Hivyo, kila KIJIJI kinashawishiwa kijenge Zahanati yake.
Diwani huyo amesema kwa sasa Vijiji vyote 3 vinatumia Zahanati moja iliyoko Kijijini Bukima. Zahanati hiyo inapanuliwa kwa kujenga WADI ya Mama na Mtoto ambapo Mbunge wao, Prof Sospeter Muhongo tayari amechangia SARUJI MIFUKO 100.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Butata, Ndugu William Mbasa  amesema ujenzi wa Zahanati ya Kijiji chao ulianza Mwaka 2018, ukasuasua, lakini kwa sasa WANANCHI WAMEAMUA kuendelea na kukamilisha ujenzi wa Zahanati hiyo.
MICHANGO inaendelea kutolewa na WANAVIJIJI, ambayo ni NGUVUKAZI (kusomba mawe, mchanga na maji) na SHILINGI 5,000/= kwa kila KAYA. Mbunge wa Jimbo, Prof Sospeter Muhongo alishachangia SARUJI MIFUKO 50 kwa ajili ya ujenzi wa msingi wa BOMA la Zahanati hiyo.
MIUNDOMBINU YA HUDUMA ZA AFYA JIMBONI
Jimbo la Musoma Vijijini lina Vijiji 68 na kwa sasa WANAVIJIJI wanajenga ZAHANATI MPYA 13 na KITUO CHA AFYA 1. Ujenzi mwingine ni wa HOSPITALI ya WILAYA na upanuzi wa Zahanati ya Kijiji cha Masinono kuwa KITUO CHA AFYA cha Kata ya Bugwema.
Kwa sasa HUDUMA ZA AFYA ndani ya Jimbo zinatolewa na ZAHANATI 24 za Serikali na VITUO VYA AFYA 2 vya Serikali. Zahanati za BINAFSI ni 4.