ZAO LA DENGU LAANZA KULIMWA KWENYE BONDE LA BUGWEMA

Ndugu Owiyo na Familia yake wakiwa kwenye palizi ya DENGU. Hapo ni Kijijini Masinono, Kata ya Bugwema.

Jumapili, 15.12.2019
Jimbo la Musoma Vijijini
Na: Hamisa Gamba
Msaidizi wa Mbunge
KATA ya BUGWEMA inayoundwa na Vijiji vinne (4) yaani Muhoji, Masinono, Kinyang’erere na Bugwema ina BONDWE kubwa kwa ajili ya Kilimo cha Mazao ya CHAKULA na BIASHARA. Kilimo kikubwa cha UMWAGILIAJI kitatekelezwa kwenye BONDE hili.
Bonde la BUGWEMA lina ukubwa wa EKARI 5,075 (hekta 2,054)
Mazao makuu ya CHAKULA yanayolimwa BUGWEMA ni: MAHINDI, MIHOGO, MTAMA, MPUNGA, VIAZI VITAMU, MATUNDA na MBOGAMBOGA.
Mazao Makuu ya BIASHARA yanayolimwa BUGWEMA ni: PAMBA, ALIZETI, MPUNGA, MAHINDI na DENGU.
DENGU ni zao JIPYA la CHAKULA na BIASHARA liloanzwa kulimwa BUGWEMA kwa miaka ya karibuni. Ni moja ya MAZAO yatakayoendelea kulimwa kwa wingi kwenye BONDE la BUGWEMA kwenye KILIMO CHA UMWAGILIAJI kitakachoendeshwa na MRADI mkubwa wa Benki ya Kilimo (Tanzania Agricultural Development Bank, TADB) kwa kushirikiana na WANAVIJIJI na HALMASHAURI ya Wilaya ya Musoma (Musoma DC). Mazao mengine ya MRADI huo ni: MPUNGA, VITUNGUU, MAHINDI, ALIZETI na PAMBA.
Mmoja ya Wakulima wa DENGU kwenye Kijiji cha Masinono, Ndugu Francis Owiyo  amesema kwamba hivi karibuni ameanza kujishughulisha na Kilimo cha DENGU. Vilevile, hulima ALIZETI. Ndugu Owiyo ambaye kwa sasa ameanza kwa kulima Ekari 3 za DENGU, amesema  kuwa zao hilo kwa  kawaida linachukua takribani miezi mitatu  (3) kuwa tayari kwa kuvunwa.
Mkulima huyo amesema KILO 1 ya DENGU huuzwa kwa bei ya Shilingi 800 – 1,000. Ndugu Owiyo anasubiri kwa hamu kubwa MRADI wa Kilimo cha UMWAGILIAJI kwenye BONDE la BUGWEMA. Anakusudia kupanua mashamba yake kwa kutumia ZANA za KISASA za KILIMO zitakazotolewa na Benki ya Kilimo (TADB).
Diwani wa Kata ya Bugwema, Mhe Ernest Magembe ameendelea kushawishi na kushauri wananchi wa Kata hiyo kuhakikisha wanaongeza juhudi kubwa kwenye Kilimo ili kutokomeza NJAA kwenye Kata yao na Jimboni kwa ujumla.
Diwani huyo ameendelea kutoa shukrani za pekee kwa Mbunge wa Jimbo, Prof Sospeter Muhongo kwa kugawa bure mbegu za MTAMA, MIHOGO, UFUTA na ALIZETI kwa Wakulima wa Kata ya Bugwema na Jimboni kote (Kata 21).
Diwani huyo ameongeza kwa kusema kwamba Wanavijiji wa Kata ya Bugwema ndio WAKULIMA MASHUHURI wa mazao ya ALIZETI na DENGU ndani ya Jimbo la Musoma Vijijini.
HATUTAKI NJAA NDANI YA JIMBO LA MUSOMA VIJIJINI – TWENDENI SHAMBANI!