SEKONDARI ZAJITAYARISHA KWA ONGEZEKO LA WANAFUNZI MWAKANI (JAN 2020): VYUMBA VIPYA VYA MADARASA VINAHITAJIKA

Wajumbe wa Baraza la Maendeleo la Kata ya Musanja wakiwa kwenye Kikao cha WDC

Na: Fedson Masawa
Msaidizi wa Mbunge
Jimbo la Musoma Vijijini lina Jumla ya Sekondari za Kata/Serikali 18 na za Binafsi 2.
Wananchi kwa kushirikiana na Serikali yao  WANAJENGA Sekondari Mpya 9.
Wananchi WAMEDHAMIRIA kwamba ifikapo Januari 2020, Sekondari Mpya zitakazochukua Wanafunzi wa Kidato cha I (FORM I) ni:
(1) Dan Mapigano Memorial Secondary School ya Kata ya Bugoji yenye Vijiji 3.
(2) Busambara Secondary School ya Kata ya Busambara yenye Vijiji 3.
(3) Nyasaungu Secondary School inayojengwa na Kijiji 1 cha Nyasaungu ndani ya Kata ya Ifulifu.
HAYO HAPO JUU NI MATAYARISHO MAZURI ya kupunguza umbali wa kutembea na msongamano madarasani wa Wanafunzi.
Vilevile, MABARAZA ya Maendeleo ya Kata (WDC) yameweka mipango maalumu ya ujenzi wa Vyumba VIPYA vya Madarasa kwa Shule za Sekondari zilizopo ili kukabiliana na mahitaji sahihi ya Januari 2020.
Oktoba 7, 2019 Wajumbe wa Baraza la Maendeleo la Kata ya Musanja (WDC) walifanya MAJADILIANO ya uharakishaji wa ujenzi wa Vyumba Vipya vitatu (3) vya Madarasa katika Sekondari yao ya Kata, Mabui Secondary School. Kikao hicho kilifanyika chini ya Mwenyekiti wa WDC, Mhe Diwani Elias Majura Ndaro.
Awali akitoa taarifa ya Shule hiyo, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mabui, Mwalimu Generose Severine alisema kuwa shule ina jumla ya Wanafunzi 304 na ina Vyumba 7 vya Madarasa.
Mwalimu Mkuu huyo alisema Sekondari hiyo inatarajia kupokea takribani Wanafunzi Wapya 157 (Form I). Kwa hiyo, patakuwepo na UPUNGUFU wa Vyumba 3 vya Madarasa. Hivyo, kuna haja ya kujenga Vyumba Vipya vitatu (3).
Kutokana na taarifa hiyo, Wajumbe wa Baraza la Maendeleo la Kata ya Musanja kwa pamoja WAMEAMUA kwamba Vijiji vyote vitatu vya Kata hiyo (Musanja, Mabui na Nyabaengere) vitaanza ujenzi huo Oktoba 16, 2019 ambapo kila Kijiji kitajenga chumba kimoja (1) cha Darasa
Katika kuboresha Miundombinu ya Shule ya Sekondari Mabui, Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Prof Sospeter Muhongo, alishachangia  Mabati 54 kwa ajili ya kuezeka chumba kimoja (1) cha darasa. Vilevile, Mbunge huyo aliwapatia Vitabu vingi vya Masomo ya Sayansi na Kiingereza.
UJENZI wa Vyumba Vipya 3 ukianza, Mbunge wa Jimbo, Prof Sospeter Muhongo ataenda hapo Shuleni kupiga HARAMBEE na yeye mwenyewe kuchangia ujenzi huo.