MBEGU YA  MIHOGO YA AINA YA MKOMBOZI YANUFAISHA WAKULIMA JIMBONI

Ndugu Ladislaus Manumbu na familia yake wakipalilia SHAMBA lao la MIHOGO lililotumia Mbegu ya MKOMBOZI. Hapo ni Kijijini Bukima.

Na: Verediana Mgoma
Msaidizi wa Mbunge
UCHUMI na AJIRA kuu kwa Wananchi wa Jimbo la Musoma Vijijini viko kwenye SEKTA za Kilimo, Uvuvi, Ufugaji na Biashara. Sekta ya KILIMO ndiyo uti wa mgongo wa UCHUMI na AJIRA kubwa zaidi kuliko hizo nyingine.
MAZAO Makuu ya CHAKULA ni MIHOGO, MAHINDI, MTAMA, VIAZI VITAMU na MPUNGA.
ZAO kuu la BIASHARA ni PAMBA  na kwa misimu mitatu hii ya kilimo (2016/17- 2018/19), zao la ALIZETI nalo limeanza kulimwa Jimboni mwetu. Kilimo cha MPUNGA na MIHOGO nacho kinasisitizwa kiwe kwa ajili ya CHAKULA na BIASHARA.
MRADI MKUBWA WA KILIMO CHA UMWAGILIAJI WA BONDE LA BUGWEMA, ulionzishwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu J.K.Nyerere, UNAFUFULIWA.
KILIMO cha UMWAGILIAJI kwenye Bonde la BUGWEMA lenye ukubwa wa Ekari 5,075 utakuwa wa Ushirika kati ya WANAVIJIJI, HALMASHAURI na BENKI YA MAENDELEO YA KILIMO TANZANIA (TADB). Mazao yatakayozalishwa kwenye Bonde hili ni: MPUNGA, MAHINDI, VITUNGUU, DENGU, ALIZETI na PAMBA.
Kijiji cha Bukima ni miongoni mwa Vijiji 68 vya Jimbo la Musoma Vijijini ambacho shughuli zake kuu za UCHUMI ni KILIMO na UVUVI.
Mazao cha Chakula ya Wakazi wa Kijiji cha Bukima ni: mihogo, viazi vitamu na viazi lishe, mahindi, mpunga, mtama na mbogamboga. Kilimo chao ni cha mazoea!
Ndugu Ladislaus Manumbu ni miongoni mwa Wakulima wachache maarufu wa ZAO la MIHOGO ambae AMEAMUA kutumia MBEGU ya MIHOGO ya aina ya MKOMBOZI.
Ndugu Manumbu anaeleza kwamba baada ya kupokea vijiti vya mihogo aina ya MKOMBOZI amefuata MAELEKEZO ya KILIMO BORA na kufanikisha kupata MAVUNO MAZURI kwa misimu mitatu mfululizo. Kila Ekari anavuna MAGUNIA kati ya 16 na 20. MBEGU za ASILI hutoa MAGUNIA kati ya 5 na 6 kwa Ekari moja. Vilevile, Mbegu ya MKOMBOZI inastahili MAGONJWA.
Baada ya MAVUNO mazuri kutoka Mbegu ya MKOMBOZI, Wanavijiji jirani wameomba na kupewa mbegu hiyo na Ndugu Manumbu. Mbegu hii ya MKOMBOZI kwa sasa inatumiwa na Wakulima wengi kwenye Jimbo la Musoma Vijijini.
Mtendaji wa Kijiji cha Bukima, Ndugu Josephat Phinehas amesema anashirikiana na Afisa Kilimo kukuza na kuboresha Kilimo cha Mihogo Kijijini Bukima.
Wananchi na Viongozi wa Kijiji cha Bukima na Vijiji vingine Jimboni wanamshukuru sana Mbunge wao, Profesa Sospeter Muhongo kwa juhudi zake za KUBORESHA  KILIMO cha Mazao ya CHAKULA na BIASHARA Jimboni mwao. Mbunge huyo AMEGAWA BURE Mbegu za ALIZETI, MTAMA, MIHOGO na ULEZI kwa Wakulima ndani ya Vijiji vyote 68 vya Jimbo hilo.