UJENZI WA SHULE SHIKIZI MWALONI KIJIJINI BURAGA UNAENDELEA VIZURI

Ujenzi wa BOMA la Vyumba Viwili (2) vya Madarasa na Ofisi 1 ya Walimu kwenye Shule Shikizi Mwaloni, Kijijini Buraga, Kata ya Bukumi.

Na: Verediana Mgoma
Msaidizi wa Mbunge
Ujenzi wa Shule Shikizi Mwaloni  kwenye Kitongiji cha Mwaloni, Kijiji cha Buraga, Kata ya Bukumi umefikia hatua nzuri ambapo Boma la Vyumba Viwili (2) vya Madarasa na Ofisi moja (1) ya Walimu limeanza kunyanyuliwa.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Buraga, Ndugu Gerald Mageta ameelezea mafanikio ya ujenzi huo kuwa, mbali na MICHANGO ya WADAU wa Maendeleo, WAKAZI wa Kitongoji wa Buraga wanachangia NGUVUKAZI zao ikiwemo kusomba mawe, mchanga na maji ya ujenzi. Vilevile wanachanga  Tsh 5,000/- (elfu tano) kutoka kila Kaya.
Baada ya kukamilisha ujenzi wa BOMA hilo kifuatacho ni ujenzi wa Matundu 4 ya Choo, Nyumba moja  ya Mwalimu na baade kuongeza Vyumba vya Madarasa kwa ajili ya kuwa na Shule ya Msingi yenye Darasa la I hadi la VII.
WAKAZI wa Kitongoji cha Mwaloni na Kijiji cha Buraga kwa ujumla wao, WANAOMBA WAZALIWA na WADAU wa Maendeleo  wajitokeze KUCHANGIA ujenzi huu – hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa Kijiji cha Buraga, Ndugu Gerald Mageta.
Kwa upande wake, Mlezi wa Shule Shikizi Mwaloni, Mwl  Robart Marwa ameiomba SERIKALI na WADAU wengine wa Maendeleo waendelee kuunga mkono jitihada za Wanakijiji hao ili waweze kuondoa tatizo la Watoto zaidi ya 80 ambao hutembea umbali wa kilomita zaidi ya 4 kwenda masomoni kwenye Shule za Msingi za jirani zilizoko Vijiji vya Chitare na Buraga.
Aidha Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Shule hiyo, Ndugu Nyajoge Nyanjara amesema kwa sasa wana jumla ya WANAFUNZI 51 wa UTAYARI ambao wanasomea chini ya  MTI kwa sababu ya UKOSEFU wa Vyumba vya Madarasa.
Wananchi wa Kitongoji cha Mwaloni na wa Kijiji chote cha Buraga WANAMSHUKURU Mbunge wao Profesa Sospeter Muhongo kwa MCHANGO wake wa SARUJI MIFUKO 50. Vilevile MFUKO wa JIMBO umewachangia SARUJI MIFUKO 50.
Shule ya Shikizi Mwaloni ni kati ya  Shule Mpya 10 (kumi) za Msingi zinazojengwa (na nyingine zimekamilisha ujenzi) Jimboni mwetu. Kwa sasa Vijiji vyetu 68 vina jumla ya Shule za Msingi 113 (111 za Serikali na 2 za Binafsi).
Jimbo la Musoma Vijijini linaelekea kwenye KILA KIJIJI  kuwa na SHULE za MSINGI MBILI (2). TUMEDHAMIRIA, TUTAFANIKIWA!