KITONGOJI CHA RWANGA CHAENDELEA KWA KASI KUBWA KUJENGA SHULE YAKE YA MSINGI 

Kikao cha Walimu wa S/M Rwanga, Wananchi wa Kitongoji cha Rwanga, Viongozi mbalimbali wa Kijiji/Kata, CCM Wilaya na Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini.

Jumatatu, 03.06.2019
Jimbo la Musoma Vijijini
Shule ya Msingi Rwanga iliyoko kwenye Kitongoji cha Rwanga, Kijijini Kasoma, Kata ya Nyamrandirira ilianza kujengwa na kufunguliwa Mwaka huo huo wa 2016.
Shule ina Madarasa 4 (Std I-IV), Walimu 5 na Mwalimu 1 wa Kujitolea. Vipo Vyumba 4 vya Madarasa, Ofisi 2 za Walimu na Choo chenye Matundu 6. Nyumba ya Mwalimu Mkuu imejengwa kwenye eneo la Shule.
Mwalimu Mkuu wa Shule, Mwl David Lawrent Swedi, Mtendaji wa Kijiji, Ndugu Phaustine Augustine na Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji, Ndugu Fedson Msalama kwa PAMOJA WANASIMAMIA kwa umakini na mafanikio makubwa ujenzi wa hiyo Shule.
Wakazi wa Kitongoji cha Rwanga WANACHANGIA NGUVUKAZI zao kwa kusomba mchanga, mawe, kokoto na maji. Vilevile, kila KAYA inachangia fedha taslim, Tshs 15,000.
Mradi wa EQUIP wa Ushirika kati ya Serikali yetu na ya Uingereza (DfID) ulitoa Tsh Milioni 25.2 kwa ajili ya ujenzi huo na kuunga mkono Wananchi waliojitolea kuboresha ubora wa ELIMU hapo Kijijini.
Mbunge wa Jimbo ameishatoa MICHANGO yake kwa S/M Rwanga kama ifuatavyo: (i) SARUJI MIFUKO 110, (ii) MADAWATI 41.
Leo, 03.06. 2019, baada ya Mbunge huyo kukagua ujenzi unaoendelea hapo Shuleni, amechangia SARUJI MIFUKO 50 ambayo itatumika kwenye ujenzi Mpya wa Vyumba vingine 2  vya Madarasa ambavyo WANANCHI wameahidi kuvikamilisha ifikapo 30.06.2019.
MFUKO wa JIMBO umechangia MABATI 150 kwenye ujenzi wa Vyumba 2 vipya vya Madarasa na Ofisi 1 ya Walimu hapo Shuleni.
Kwa kuwa Shule sasa inazo Ofisi za Walimu, Mbunge wa Jimbo amewapatia VITABU vya Elimu ya Shule ya Msingi. Vilevile Mbunge huyo  AMECHANGIA sehemu ya posho ya Mwalimu wa Kujitolea wa S/M Rwanga.
Viongozi wa CCM Wilaya ya Musoma Vijijini (Makatibu: UWT, WAZAZI na UVCCM) na Mwenyekiti WAZAZI Wilaya wameshiriki kwenye UKAGUZI wa ujenzi huo. Wameongozwa na Katibu wa CCM Wilaya, Ndugu Stephen Koyo,
Diwani wa Kata ya Nyamrandirira, Mhe Maregesi,  AMEWASHUKURU sana Wananchi na Wadau wa Maendeleo, ikiwemo Serikali yetu, kwa KUCHANGIA ujenzi wa Shule hiyo Mpya kwenye Kata yao. Amewaomba Wazaliwa wa Kata ya Nyamrandirira yenye Vijiji 5, WAJITOKEZE kuchangia ujenzi wa Seka Secondary School unaoendelea Kijijini Seka.