WANANCHI WA KIJIJI CHA KABEGI  WAAMUA KUJENGA SHULE SHIKIZI KWENYE KITONGOJI CHA BINYAGO

Maboma ya Vyumba vya Madarasa ya Shule SHIKIZI kwenye Kitongoji cha Binyago, Kijijini Kabegi.

Na:Verediana Mgoma
Msaidizi wa Mbunge
Jumatatu, 15.04.2019
Jimbo la Musoma Vijijini
Wananchi wa Kijiji cha Kabegi, Kata ya Ifulifu WAMEAU  KUJITOLEA na KUCHANGIA ujenzi wa Shule SHIKIZI kwenye Kitongoji cha Binyago.
Mradi huu ulianzishwa na WAKAZI wa Kitongoji cha Binyago. Baadae Serikali ya Kijiji cha Kabegi yenye Shule ya Msingi moja tu ILIAMUA MRADI huu upanuliwe kwa lengo la kujenga Shule ya Msingi ya pili. Kwa hiyo hatua ya kwanza ni kuanza na ujenzi wa Shule Shikizi na hatua ya pili ni kujenga Shule ya Msingi inayojitegemea.
Watoto wadogo wa Kitongoji cha Binyago hutembea umbali mrefu wa takribani kilomita sita (6) kwenda Kijiji jirani masomoni kwenye  Shule ya Msingi Nyasurura.
Mtendaji wa Kijiji cha Kabegi, Ndugu Pili Thomas amesema kwamba Kijiji cha Kabegi kina Kaya 390 na kila Kaya IMEKUBALI KUCHANGIA Shilingi Elfu Kumi (Tsh 10,000) kwa ajili ya ujenzi wa Vyumba vya Madarasa vya Shule SHIKIZI yao.
Maboma ya Vyumba Viwili (2) na Ofisi ya Walimu yako tayari KUEZEKWA.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kabegi, Ndugu Charles Toto amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Profesa Sospeter Muhongo kwa kuwaunga mkono Wananchi kwa kuchangia SARUJI MIFUKO 50.
Vilevile wanashukuru kupokea SARUJI MIFUKO 50 kutoka Fedha za Mfuko wa Jimbo.
Ndugu Toto amesema kwamba Mifuko hiyo 100 ya Saruji imeongeza hamasa yao ya kuchangia ujenzi wa Shule Shikizi kwenye Kitongoji chao.
Kiongozi huyo aliendelea kusema kuwa wana MPANGO  wa kuongeza  Vyumba vya Madarasa, kujenga Choo chenye Matundu nane (8) na Nyumba ya kuishi Walimu.
Wananchi wa Kijiji cha Kabegi WANAOMBA Wadau wa Maendeleo wawaunge mkono na kuwachangia, SARUJI, MABATI na MBAO za kukamilisha ujenzi wa Shule hiyo SHIKIZI ambayo hatimae itakuwa Shule ya Msingi inayojitegemea na kufanya Kijiji cha Kabegi kuwa na Shule za Msingi mbili (2).