JIWE LA MSINGI LA “DAN MAPIGANO MEMORIAL SECONDARY SCHOOL” KUWEKWA TAREHE 18.04.2019

MAJENGO ya Dan Mapigano Memorial Secondary School ya Kata ya Bugoji. yamefikia hatua nzuri.

Na: Hamisa Gamba
Msaidizi wa Mbunge
Wananchi wa Kata ya Bugoji Jimboni Musoma Vijijini, wameendelea na ujenzi wa Sekondari yao ya Kata kwa kasi na umakini mkubwa sana.
Sekondari hiyo imepewa jina la “Dan Mapigano Memorial Secondary School”
kwa nia ya kumuenzi Msomi, Mwanasheria mahiri na Jaji wa Mahakama Kuu wa kwanza kutoka Jimbo la Musoma Vijijini. Marehemu Jaji Dan Mapigano alizaliwa Kijiji cha Bugoji.
Kwa sasa Wanafunzi wa Sekondari kutoka Kata ya Bugoji yenye Vijiji 3 (Kaburabura, Kanderema na Bugoji) na Kata ya Nyambono yenye Vijiji 2 (Saragana na Nyambono) wote wanasom kwenye Sekondari ya Nyambono – umbali wa kutembea ni mkubwa, Vyumba vya Madarasa havitoshi, Maabara haijakamilika.
Kwa hiyo Kata ya Bugoji imeamua kujenga Sekondari yake ili KUBORESHA MAZINGIRA ya kujifunza na kufundisha MASOMO ya Sekondari kwa Wanafunzi wa Kata zote mbili.
Akieleza juu ya Ujenzi wa Sekondari hiyo, Diwani wa Kata ya Bugoji,  Mhe Ibrahim Malima amesema tangu ujenzi huo ulipoanza rasmi Mwezi Desemba 2018, unaendeshwa kwa NGUVU za WANANCHI, SERIKALI, MBUNGE wa JIMBO na WADAU wengine wa  Maendeleo kwa mchanganuo ufuatao:
(i) SERIKALI (TAMISEMI):  imetoa Tsh 62.5 Milioni ambazo zitakamilisha Ujenzi wa Vyumba 5 vya Madarasa
(ii) MFUKO wa Jimbo: Saruji Mifuko 75
(iii) MBUNGE wa Jimbo: Saruji Mifuko 50 na anaendelea kuchangia
(iv) WAZALIWA wa Kata ya Bugoji nao wanachangia, orodha ni ndefu –  Diwani Malima, Injinia Nyamuhanga, Mkwaya Toto Songorwa, Mafuru Kaitira, Petro Mfungo, Raphael Magoti, Parapara Bulenga, Kabende Manyama,  Mshangi Kaitira, Munepo Machumu na wengine wanazidi kujitokeza kuchangia ujenzi wa Sekondari ya Kata yao.
Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Bugoji ambaye pia ni Kaimu WEO wa Kata ya BUGOJI, Ndugu Ernest Maregesi ametoa SHUKRANI NYINGI kwa Wananchi wa Kata hiyo kwa kuwa ndio waanzilishi wa ujenzi huo, Serikali, Mbunge na Wadau wengine wa Maendeleo kwa kuungana pamoja hadi kufikia hatua hiyo kama ifuatavyo:
(i) Boma la Vyumba viwili (2) limekamilika na hivi karibuni wanaanza kupaua baada ya kukamilisha ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Shule na Makamu wake. Ofisi hizi 2 ziko kwenye Jengo hilo.
(ii) Boma lingine la Vyumba viwili (2) na Ofisi 1 wanafunga renta, huku wakiendelea na ufyatuaji wa matofari ili kuanza ujenzi wa Vyumba vingine vya Madarasa na Nyumba ya kuishi Walimu.
Dan Mapigano Memorial Secondary School itafunguliwa rasmi Januari 2020 na kuanza kuchukua Wanafunzi wa Form I.
Jiwe la Msingi litawekwa siku ya Alhamisi, tarehe 18.04.2019, saa 4 asubuhi, Kijijini Bugoji. KARIBUNI WOTE