WANANCHI KIJIJI CHA CHIMATI WAAMUA KUJENGA ZAHANATI YA KIJIJI CHAO

Kazi za ujenzi wa ZAHANATI Kijiji cha Chimati

15.03.2019
Na: Verediana Mgoma
Msaidizi wa Mbunge
Wananchi Kijiji cha Chimati, Kata ya Makojo wameamua KUJITOLEA kujenga ZAHANATI ndani ya Kijiji chao. UAMUZI huu umefikiwa baada ya Wanakijiji hao kuchoshwa na adha ya kutembea umbali mrefu kufuata HUDUMA ya AFYA Kijiji cha Jirani cha Chitare.
Ndugu Juma Nyituga, Mtendaji wa Kijiji cha Chimati amesema kuwa jumla ya WAKAZI 535 wanalazimika kutembea umbali wa kilomita 10  kufuata HUDUMA ya AFYA katika Kijiji cha Chitare. Kwa hiyo wameamua kujenga Zahanati kijijini mwao ili kutatuta tatizo hilo.
Akizungumzia Ujenzi wa Zahanati hiyo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Chimati, Ndugu Masinde Bwire amesema kuwa  kukamilika kwa ZAHANATI hiyo kutaboresha HUDUMA za AFYA Kijijini hapo. Mama Wajawazito, Watoto na Wazee hawatapata usumbufu wa kutembelea umbali mkubwa kama ilivyo sasa.
Mkuu wa Wilaya ya  Musoma Dkt. Vicent Anney amewapongeza Wananchi wa Kijiji cha Chimati na kuwaomba wakamilishe ujenzi wa Zahanati yao mapema iwezekanavyo na vilevile amewashauri  waendelee kuunga mkono SERIKALI kwenye MIRADI ya MAENDELEO yao. Mkuu wa Wilaya huyo alisema Ujenzi wa ZAHANATI hiyo kwa mtindo wa KUJITOLEA ni mfano wa kuigwa na Vijiji vingine.
Aidha sambamba na jitihada hizo za Wananchi Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Prof Sospeter Muhongo ametoa MCHANGO wa SARUJI MIFUKO 50 akichangia ujenzi wa Msingi (foundation) na akatoa  ahadi ya kuchangia SARUJI MIFUKO mingine 50 wakati wa Ujenzi wa Boma la Zahanati hiyo.
MICHANGO MINGINE mikubwa  aliyokwishatoa Mbunge Prof Muhongo kwenye Kijiji cha Chimati na kwenye Vijiji vingine vya Kata ya Makojo ni: SARUJI, MABATI, MADAWATI, VITABU, MBEGU za Alizeti, Mihogo na Mtama.
Michango hiyo imetolewa na Mbunge wa Jimbo ili kuunga mkono juhudi za Wanavijiji kwenye Utekelezaji wa MIRADI yao ya KIPAUMBELE ya ELIMU, AFYA na KILIMO.