WANANCHI WA KIJIJI CHA CHIMATI WAMEAMUA KUPUNGUZA UHABA WA VYUMBA VYA MADARASA

UJENZI wa Vyumba vya Madarasa kwa njia ya KUJITOLEA, katika Shule za Msingi Chimati A na Chimati B

Na: Verediana Mgoma, Msaidizi wa Mbunge
19.11.2018
WANANCHI wa Kijiji cha Chimati,  Kata ya Makojo wameendelea KUTATUA TATIZO SUGU LA UPUNGUFU wa Vyumba vya Madarasa katika Shule za Msingi mbili (2) za Kijijini mwao, yaani S/M Chimati A na S/M Chimati B, kwa kuboresha Miundombinu ya Elimu ikiwa ni pamoja na UJENZI wa Vyumba vya Madarasa kwa njia ya KUJITOLEA.
Akitoa taarifa za UJENZI wa Vyumba vya Madarasa Shuleni hapo, Mtendaji wa  Kijiji cha Chimati, Ndugu Juma Chacha alimueleza Msaidizi wa Mbunge kuwa WANANCHI wa Kijiji cha Chimati WAMEAMUA KUJITOLEA KUJENGA Vyumba vya Madarasa ili kupunguza na hatimae KUTATUA TATIZO la UPUNGUFU wa Vyumba vya Madarasa kwenye Shule zao mbili (2) za Msingi.
Ndugu Chacha ameongezea kuwa, kutokana na MPANGOKAZI wa UJENZI huo, wamekubaliana KILA KITONGOJI kujenga chumba kimoja cha Darasa ambapo mpaka sasa WAMEFANIKIWA kujenga Vyumba 4 kwa MICHANGO na NGUVU zao wakisaidiwa na WAFADHILI mbalimbali.
Nae Mwenyekiti wa Kijiji, Ndugu Masinde Ndege alimshukuru sana Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Prof. Sospeter Muhongo  kwa MCHANGO wake wa SARUJI MIFUKO 60 iliyotumika kwenye UJENZI wa Vyumba Vitatu (3) vya Madarasa
MCHANGO mwingine ulitoka kwenye MFUKO wa JIMBO (fedha zake zinatunzwa na Halmashauri) uliochangia MABATI 54 yaliyotumika kuezeka Chumba kimoja cha Darasa.
Wananchi wa Kijiji cha Chimati wanaendelea kumshukuru Mbunge wao kwa KUCHANGIA MADAWATI 146 kwa Shule zote mbili (2) za Msingi.
Mwenyekiti wa Kijiji  cha Chimati, Ndugu  Masinde Ndege ANAWAOMBA WADAU wa MAENDELEO na WAZALIWA wa Kijiji cha Chimati waishio nje ya Kijiji hicho KUJITOLEA KUCHANGIA ujenzi huo ili ukamilike mapema.
KARIBUNI TUCHANGIE MAENDELEO YETU KWA VITENDO na kwa KUSHIRIKIANA na SERIKALI YETU