VIKUNDI VYA BUSTANI KUTOA FURSA ZAIDI ZA KILIMO CHA UMWAGILIAJI

Vijana wa Kikundi cha No Sweat No Sweet cha Kijijini Bugunda wakiwa wanaendelea na kazi za Uzalishaji kwenye bustani yao

Na Verediana Mgoma, Msaidizi wa Mbunge
VIKUNDI vya Kilimo cha Umwagiliaji ndani ya Jimbo la Musoma Vijijini vimejipanga kutoa ELIMU itakayohamasisha VIJANA na AKINA MAMA  kuchangamkia fursa za KILIMO cha UMWAGILIAJI hasa kwa jamii zinazoishi karibu na vyanzo vya maji mengi yanayoweza kutumika kwenye umwagiliaji.
Hayo yamezungumzwa mapema wiki hii na Ndugu Gudluck Wambwe ambaye ni Mwenyekiti wa Kikundi cha NO SWEAT NO SWEET cha Kijijini Bugunda, Kata ya Bwasi.
Kikundi hicho cha Kijijini Bugunda, kwa kipindi kirefu kimekuwa kikijishughulisha na Kilimo cha Bustani za Mbogamboga na Matunda.
Ndugu Gudluck Wambwe alisema kuwa, wamekuwa wakipata maarifa ya Kilimo cha Umwagiliaji kutoka kwa  Mtaalamu wa Kilimo wa Kata yao.
Ameongezea kuwa “Kupitia Kilimo cha Umwagiliaji tayari wamekwishanufaika na faida za Kilimo hicho ni nyingi zikiwemo: kuwa na uwezo wa kifedha wa kugharimia mahitaji ya shule ya watoto wao, na kujipatia mahitaji mbalimbali ya kifamilia.”
Aidha, Kiongozi huyo alisema kuwa, malengo yao ya sasa ni kuielimisha jamii kuhusu Kilimo cha Umwagiliaji tofauti na ilivyozoeleka hapo awali kujikita kwenye Kilimo cha Asili (msimu wa mvua) peke yake.
Kwa upande wake Afisa Kilimo wa Kata, Ndugu Gustav Tesha alieleza kuwa, anaendelea kuwapa elimu wakazi wa Kata za Bulinga na Bwasi juu ya Kilimo cha Umwagiliaji na anakiri kwamba jamii imekubali kubadilika na kuwa na mtazamo mpya wa kushiriki katika Kilimo cha Umwagiliaji.
Ikumbukwe kuwa, Kikundi cha NO SWEAT NO SWEET ni moja kati ya Vikundi 15 vilivyofadhiliwa Pampu, Mipira ya umwagiliaji na Mbegu kutoka kwenye Mgao wa FEDHA ZA MFUKO WA JIMBO awamu ya kwanza.
Wanakikundi na Washiriki wa Kikundi cha NO SWEAT NO SWEET wanamshukuru Mbunge wao Prof. Muhongo kwa juhudi zake za kuipa kipaumbele Sekta ya Kilimo cha Kisasa na chenye Manufaa ili kuinua Uchumi wa Wananchi wa Jimbo la Musoma Vijijini na wanasema kwao Kilimo ni Ajira.