KILIMO CHA KISASA CHA WANANCHI WENYEWE NDANI YA BONDE LA BUGWEMA

Wananchi wa kijiji cha Bugwema na vijiji jirani vya Kata ya Bugwema na Kata za jirani wakimsikiliza kwa makini Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Mhe Dkt Vincent Naahano katika mkutano uliohusu MRADI wa UWEKEZAJI wa BENKI YA MAENDELEO YA KILIMO Tanzania ndani ya Bonde la Bugwema.

Na Hamisa Gamba, Msaidizi wa Mbunge.
Alhamisi, tarehe 27.09.2018, saa 4 asubuhi, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Mhe Dkt Vincent Naahano ALIFANYA MKUTANO  na WANANCHI wa Kijiji cha Bugwema, na kuongelea juu ya MRADI wa UWEKEZAJI wa  BENKI YA MAENDELEO YA KILIMO Tanzania ndani ya Bonde la Bugwema.
Uwekezaji utakuwa wa KILIMO CHA UMWAGILIAJI kwenye SHAMBA LA BUGWEMA.
Mahudhurio kwenye Mkutano huo yalikuwa mazuri sana ambapo WANANCHI walitoka Kijiji cha Bugwema na VIJIJI JIRANI vya Kata ya Bugwema na Kata za jirani. Vilevile Watendaji wa Serikali Kata na Vijiji, na Viongozi wa Chama (CCM) walihudhuria Mkutano huu.
Imeelezwa kuwa moja ya shughuli kubwa zitakazoendeshwa na MRADI huu ni kwamba, Mwekezaji ambaye ni Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania ITAJENGA MIUNDOMBINU ya UMWAGILIAJI kwa ajili ya WANANCHI kufanya KILIMO cha UMWAGILIAJI ndani ya Bonde la Bugwema. Aidha Mwekezaji atatoa vifaa vya Kilimo kwa wananchi kwa MAKUBALIANO ya MKATABA baina ya pande zote mbili. Utaratibu wa kurejesha MIKOPO utahakikisha unawanufaisha WAKULIMA watakaokuwa ndani ya MRADI HUU.
Pembejeo zitakazotolewa na Benki ya Kilimo ni: ZANA za KISASA za Kilimo,  MBEGU, MBOLEA  na huduma nyiingine pale zitakapokuwa zinahitajika.
MAZAO MAKUU ya kuanzia yatakayolimwa kwa wingi ni MPUNGA, MAHINDI na VITUNGUU.
Kwa AWAMU YA KWANZA YA MRADI wanufaikaji watakuwa WANANCHI wa Bugwema na kadri MRADI utakapokuwa unaendelea, WANANCHI WENGINE (nje ya Bugwema) watakaribishwa kushiriki katika shughuli hizo za kilimo.  HATIMAE GHARAMA ZA MWEKEZAJI ZIKIRUDI MRADI UTAKABIDHIWA KWA WANANCHI chini ya usimamizi wa Halmashauri yao.
Kwa taarifa hiyo ya Mkuu wa Wilaya (DC),  wananchi wamekubali na kuupokea MRADI huo kwa furaha kubwa, huku wakithibitishiwa na Mhe DC kuendelea kuyatumia mashamba waliokuwa wamelima mwaka jana ndani ya BONDE HILO.
Eneo lingine katika BONDE (SHAMBA) hilo la Bugwema la  zaidi ya EKARI 800 WAMEPEWA WAKAZI wa Bugwema kwa ajili ya MALISHO ya mifugo yao, na KUJENGA Shule, Zahanati na Ofisi ya Serikali ya Kijiji na Taasisi nyingine za Serikali.
Bugwema mambo ni moto, wananchi wanafurahishwa na Uongozi mzuri unaofanywa na Viongozi wa Wilaya ya Musoma (Halmashauri, Jimbo, Kata na Vijiji) wa kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma stahiki na Maendeleo chanya.
Picha hapo chini zinaonyesha DC wa Wilaya ya Musoma akiwa na Wananchi na Viongozi mbalimbali waliokuwa kwenye Mkutano wa leo wa Kijijini Bugwema.