KIJIJI CHA BUTATA CHAEZEKA CHUMBA KINGINE CHA DARASA KWA KUTUMIA  MCHANGO WA FEDHA ZA MFUKO WA JIMBO

KAZI za Uezekaji wa Chumba cha DARASA la Shule ya Msingi Butata

Na Verediana Mgoma, Msaidizi wa Mbunge
Uongozi wa Shule ya Msingi Butata kwa kushirikiana na WANANCHI na Serikali ya Kijiji cha Butata wamefanikisha zoezi la uezekaji wa Chumba kingine cha DARASA baada ya kupokea Mchango wa Mabati 54 kutoka kwenye Fedha za Mfuko wa Jimbo ili kuendeleza jitihada za kupunguza tatizo la uhaba wa madarasa na MSONGAMANO wa WANAFUNZI madarasani.
Awali, akizungumza na Mwandishi wa Habari hizi, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Butata, Ndugu Cleophance Kasara alieleza kuwa
“Serikali ya Kijiji chetu kwa kushirikiana na WANANCHI inaendelea na zoezi la Ujenzi wa VYUMBA VYA MADARASA ili kupunguza tatizo hilo Shuleni hapo.”
Aidha, Mwenyekiti huyo ameongezea kuwa ataendelea KUHAMASISHA Wananchi wake kujitolea ili kufanikisha shughuli za MAENDELEO KIJIJINI humo.
Naye Kaimu Mtendaji wa Kijiji cha Butata, Ndugu Mushangi Salige amefafanua kuwa, MWAMKO wa WANANCHI wa Kijiji hicho katika Ujenzi wa Vyumba Viwili (2)  vya MADARASA umekuwa msaada mkubwa kwa WANAFUNZI ambao awali walikuwa wakisomea nje. Jua kali na mvua vilikuwa kero kubwa.
Diwani wa Kata ya Bukima, Mhe January Simula ameshukuru na kuiomba SERIKALI YETU iendelee kuwaunga mkono ili kufanikisha suala la MAENDELEO.
Mhe Diwani Simula ametoa shukrani zake kwa Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Prof Muhongo kwa msaada wa SARUJI MIFUKO 60 iliyojenga Vyumba Viwili (2) vya Madarasa na Mabati 108 (54 kutoka Mfuko wa Jimbo na 54 kutoka kwa Mbunge) ambayo yote yametumika kuezeka Vyumba hivyo vya Madarasa.
Sambamba na Michango hiyo, Shule ya Msingi Butata A na B zimeshapokea Jumla ya Madawati 86 kutoka kwa Mbunge Prof Muhongo, mchango uliomaliza kabisa uhaba wa Madawati Shuleni hapo kulingana na mahitaji ya wakati huo.