UJENZI WA ZAHANATI VIJIJINI KWA NJIA YA KUJITOLEA WAPAMBA MOTO

Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Prof Sospeter Muhongo akikagua ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Kigera Etuma

Na Fedson Masawa, Msaidizi wa Mbunge

Ujenzi wa zahanati umezidi kupamba moto katika vijiji mbalimbali vya vya Jimbo la Musoma Vijijini ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (2015-2020).

Hatua hiyo imefikiwa ikiwa ni matokeo ya hamasa kubwa kutoka kwa wananchi wa Musoma Vijijini walioamua kuungana na serikali, viongozi wao na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kusogeza huduma ya afya kwa kila kijiji Jimboni humo.

Awali akiungana na wananchi, viongozi na wadau mbalimbali wa maendeleo Jimboni mwake  Mei 1, 2018, Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Prof Sospeter Muhongo alishirikiana na Madiwani na wakazi wa kijiji cha Kurwaki na kijiji cha Kigera Etuma na kufanikiwa kuchangia zaidi ya mifuko 350 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Kurwaki kata ya Mugango na mifuko 150, nondo na misumali katika zahanati ya Kigera Etuma kata ya Nyakatende.

Akitoa taarifa ya ujenzi wa zahanati ya Kigera Etuma, mtendaji wa kijiji hicho ndugu Antony Ndege alisema, wachangiaji wa ujenzi wa Kijiji cha Kigera Etuma ni Wafadhili,Halmshauripamoja na wakazi wa kijiji hicho na tayari jengo la matibabu (OPD) limekamilika kwa asilimia 80 na nyumba ya Mganga na Muuguzi (two in one)  inajengwa kwa kasi kubwa.

Mtendaji ameongezea kuwa “malengo ya wananchi na serikali ya kijiji cha Kigera Etuma  ni kukamilisha ujenzi huo mapema ifikapo Desemba 2018  zahanati hiyo iwe imeanza kazi”

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Musoma na Diwani wa kata ya Mugango Mhe Charles Magoma kwa niaba ya wananchi amemshukuru Mbunge na wananchi wa Jimbo la Musoma Vijijini kwa kuungana kufanimisha miundombinu ya Elimj, Afya na Kilimo Jimboni.