MBUNGE MUSOMA VIJIJINI AWATEMBELEA WAHANGA WA KIMBUNGA

Mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo (katikati aliyevaa fulana ya bluu) akiwa katika shule ya msingi Bukumi ambapo vyumba vitatu vya madarasa paa zake zimeezuliwa na upepo mkali ulioambatana na mvua. Kulia kwake ni Diwani wa viti maalum kata ya Mgango Kadogo Kapi wakiwa na Diwani wa Kata ya Bukumi John Manyama.

Na Verdiana Mgoma

MBUNGE wa Jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo amezitembelea kaya zilizopatwa na matatizo ya nyumba zao kuezuliwa na upepo na nyingine kubomoka kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali Jimboni humo.

Kwenye ziara yake aliyoianza Machi 15, 2018, Prof. Muhongo ameshuhudia kaya 86 zikiwa zimekumbwa na matatizo hayo na kusababisha baadhi ya familia kukosa makazi.

Mbali na kutembelea kaya hizo na kutoa pole, mbunge huyo alitembelea shule ya msingi Bukumi iliyopo kijiji cha Bukumi ambapo ameshuhudia vyumba vitatu vya madarasa paa zake zikiwa zimeezuliwa na upepo na mashamba ya pamba yenye takribani hekari 200 yaliyoharibiwa vibaya na mvua ya mawe katika kijiji cha Bugwema.

Akizungumza na wananchi waliokumbwa na matatizo hayo, Prof. Muhongo amewataka kuwa watulivu wakati viongozi wakiendelea kufanya tathimini ya uharibifu uliotokea na kuwasihi wasitegemee msaada kutoka serikalini peke yake kwani suala hilo ni la jamii nzima kwa kushirikiana na serikali.

“Kuweni wavumilivu, viongozi na wasaidizi wangu watapita na kuchukua tathimini ya madhara yaliyotokea. Pia tambueni, serikali peke yake haiwezi kutoa msaada kwa kila mtu. Kilichopo ni ninyi wananchi na sisi kujipanga tuone tutalitatuaje hili” alisema Prof Muhongo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi wa maeneo yaliyopata tatizo hilo mbali na kusikitishwa na matukio hayo yanayojirudia kila mara, walimpongeza mbunge wao na uongozi wa Halmashauri ya Musoma kwa kuwatembelea na kuwapa pole.

“Tunamshukuru sana Prof. Muhongo na viongozi wenzake wa halmashauri kwa kuguswa na kutufikia wananchi wao kwa wakati hasa tunapopatwa na matatizo ya aina hiyo” alisema Furaha Sumuni.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Musoma Charles Magoma alisema, ili kupunguza matatizo ya mara kwa mara, wameshaagiza kila kaya kupanda miti 40, shule miti 500 na zahanati miti 100 kwa kila mwaka huku akikazia kuwa zoezi hilo ni la lazima.