PROF. MUHONGO ASAIDIA MATIBABU YA FAMILIA ILIYONG’ATWA NA MBWA

Na Hamisa Gamba

MBUNGE wa Jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo amesaidia matibabu ya chanjo kwa kumi wa familia moja waliopatwa na tatizo la kung’atwa na mbwa katika kijiji cha Bugwema, kata ya Bugwema na kusababisha vifo vya watu wawili.

Wakati alipotembelea familia hiyo, mmoja wa ndugu Samwel Onunda, alimuomba mbunge kuwasaidia matibabu na chanjo ili kuokoa maisha ya wanafamilia hao kutokana na madhara waliyoyapata baada ya kushambuliwa na mbwa na kusababisha majeruhi na vifo vya watu wawili Charles Gilbetus na Martin Gilbetus..

Akijibu maombi hayo, Prof. Muhongo alisema atasaidia matibabu ya wahanga hao, huku akiiomba jamii kuchukua tahadhari na magonjwa mlipuko yanayosababishwa na wanyama hao.

Kwa upande wake diwani wa Kata ya Bugwema Ernest Maghembe na viongozi wengine wa eneo hilo wameahidi kushirikiana na Mbunge kuhakikisha familia hiyo inapata matibabu ya kuzuia maambukizi ya magonjwa yanayosababishwa na mbwa.

Naye Musa Oyugi alitoa shukrani kwa Mbunge wa Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo kwa jinsi alivyojitolea kunusuru uhai wa wananchi wake.