KIKUNDI CHA AKINAMAMA WA LYASEMBE WAFURAHIA MAFANIKIO KWENYE KILIMO

Baadhi ya akinamama wa Kikundi cha kijiji cha Lyasembe wakiwa kwenye picha ya pamoja na Msaidizi wa Mbunge, Verdiana Mgoma alipowatembelea kwenye eneo wanalofanya mradi wao wa kilimo.

Na. Verdiana Mgoma

KIKUNDI cha akina mama wa kijiji cha Lyasembe wamesema wamepata mafanikio makubwa kiuchumi baada ya kujitosa kwenye kilimo cha umwagiliaji.

Kikundi hicho ambacho ni miongoni mwa vikundi vilivyopata ufadhili wa fedha za mfuko wa jimbo, kinajishughulisha na kilimo cha bustani za mboga mboga na matunda.

Katibu wa kikundi hicho Mawazo Jumbura alisema, baada ya kupokea mashine, mipira na mbegu kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji, walitambua kuwa wana jukumu kubwa katika jamii yao na kuamua kutumia vifaa hivyo kutafuta maendeleo yao, familia zao na jamii inayowazunguka.

Katibu huyo alisema, tangu wameanza kilimo hicho, hali zao kimaisha zimebadilika na wanamudu mahitaji ya familia zao ikiwemo kusomesha watoto na kununua mahitaji yao binafsi na wamejiwekea malengo ya kununua mashine nyingine za umwagiliaji na kuanzisha miradi mingine mbali na kilimo ili kujiongezea kipato zaidi.

Mbali na faida walizopata kupitia kikundi hicho, Katibu huyo pia ameelezea changamoto zinazowakabili ikiwa ni pamoja na ukosefu wa eneo kubwa la kulima, ukosefu wa soko la kuuzia bidhaa zao baada ya kuvuna, ugumu wa upatikanaji wa elimu kupitia matamasha, wahamasishaji na maonyesho kwa ajili ya kuboresha zaidi kilimo chao.

Hata hivyo, licha ya changamoto hizo wamemshukuru Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Prof. Sospeter Muhongo kwa kuwaonyesha fursa hiyo ya kilimo cha umwagiliaji ambacho wanaamini kitawainua kiuchumi.

Naye, Afisa kilimo wa Kata ya Murangi Maricha Mgono akizungumza kijijini Lyasembe alisema, mpango wa kilimo cha umwagiliaji ni harakati zilizowekwa kuhakikisha akina mama na vijana wanajiajiri kupitia kilimo na kuinua hali zao kiuchumi.

Mgono alisema, hivi sasa kumekuwepo na muamko mkubwa wa kilimo cha umwagiliaji katika kata hiyo tofauti na ilivyokuwa awali wakazi wa eneo husika walijikita zaidi kwenye uvuvi.

“Tumefanya jitihada za kuhamasisha uundwaji wa vikundi kwa maendeleo ya akina mama na vijana ili kuwepo kwa upatikanaji wa mikopo itakayowasaidia kuwainua kiuchumi na kufungua miradi mbalimbali” alisema.

Kwa upande wake Mtendaji wa kijiji cha Lyasembe Chikonya Chikonya alisema, kadri siku zinavyokwenda, mwitikio wa wananchi kwenye kilimo unazidi kutokana na hamasa ya Prof. Muhongo ambaye aliwahimiza kujikita kwenye kilimo hicho cha umwagiliaji na kuacha kutegemea mvua ambazo hazina uhakika kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi.

“Kijijini hapa nimepokea mbegu za mtama, mihogo, alizeti kutoka ofisi ya mbunge na mpaka sasa kuna mikakati ya kilimo cha ufuta, kwa ujumla muitikio wa kilimo kwa wakazi wa eneo hili unakuwa siku hadi siku” alisema Chikoya.