WANAFUNZI WANYERE ‘A’ WAELEZEA CHANGAMOTO YA UPUNGUFU WA MADARASA

Na Hamisa Gamba

WANAFUNZI wa shule ya msingi Wanyere A, iliyopo kata ya Suguti, Jimbo la Musoma vijijini wanakabiliwa na uhaba wa mkubwa wa vyumba vya madarasa hali inayowalazimu kusoma wakiwa chini ya miti.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi shuleni hapo, wanafunzi wa darasa la tano wa shule hiyo walisema, hivi sasa hawana tatizo la madawati kama ilivyokuwa mwanzo, lakini wanakabiliwa na uhaba wa vyumba vya madarasa.

Mmoja wa wanafunzi hao Jackson Malima alisema, mbali na changamoto ya ukosefu wa vyumba vya madarasa inayowafanya wasome kwenye mazingira magumu ikiwemo kuchomwa na jua kwa muda wote wa masomo, lakini bado darasa lao hilo la nje halina ubao wa kufundishia.

“Madarasa tuliyonayo ni machache sana, hivyo inatulazimu wakati mwingine kubadilishana chumba cha darasa na wanafunzi wa darasa lingine pale tunapohitaji kujifunza kwa maandishi hususani somo la hisabati ambalo ni lazima ubao utumike” alisema Malima.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Wanyere ‘A,’ Buriro  Manyama, alisema ukosefu wa madarasa ni changamoto kubwa inayowakabili shuleni hapo na kuchangia kwa kiasi kikubwa kushusha kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wao.

Mwalimu Manyama alisema, sambamba na hilo bado shule yao haina vyoo, hivyo huwalazimu kuchangia choo cha shule ya msingi Wanyere ‘B,’ ambacho hakikidhi mahitaji ya wanafunzi 900 wa shule zote mbili.

Kutokana na hali hiyo, wanafunzi na mwalimu mkuu huyo waliomba msaada wa serikali, viongozi na wazazi ili kukabiliana na changamoto hizo za upungufu wa vyumba vya madarasa na vyoo.