WACHIMBAJI WADOGO WAELEZA CHANGAMOTO ZINAZOWAKABILI

Wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu katika mgodi wa Karusenyi kijiji cha Suguti, Musoma vijijini wakiwa kwenye picha ya pamoja na Mkurugenzi wa mgodi huo Mapigano Peter (mwenye fulana nyeusi).

Na. Verdiana Mgoma

WANANCHI wa Jimbo la Musoma vijijini wanaojishughulisha na uchimbaji wa madini aina ya dhahabu, wameiomba serikali kuwasaidia kutatua changamoto wanazo kumbana nazo hasa kwenye sekta ya uchimbaji ili kufanya shughuli zao kwa ufanisi zaidi.

Mkurugenzi wa mgodi wa Karusenyi Mapigano Peter alisema, Jumuiya ya wachimbaji wadogo wana changamoto nyingi endapo serikali itazitatua, watafanya kazi zao kwa ufanisi, mzunguko wa fedha utaongezeka na maisha ya wachimbaji wadogo yatabadilika.

Katibu wa wachimbaji wadogo Hatari Bwatwa, alizitaja changamoto zinazowakabili kwenye shughuli zao za uchimbaji ikiwemo ugumu katika mchakato wa kupata ruzuku, ambapo inachukua muda mrefu kupata mkopo jambo ambalo linawakatisha tamaa na kuomba muda upunguzwe ili waweze kupata mikopo hiyo.

Mbali na hilo, Bwatwa alisema kutokana na kukosa mitaji, wanashindwa kupata pampu za maji zenye uwezo wa kutoa maji haraka wakati uchimbaji unaendelea, mashine za kisasa za kupasulia miamba (Jack harmmers na Compressor) ambavyo vinahitaji uwekezaji mkubwa.

“Tunahitaji crane kwa ajili ya kutoa mwamba au udongo wenye dhahabu hivisasa wachimbaji wanatumia ndoo ambapo wanatumia nguvu na muda mwingi. Pia tunakosa elimu ya kitaalamu kuhusu uchimbaji tofauti na walio wengi kutumia uzoefu” alisema Bwatwa.

Aidha, mbali na changamoto hizo za vifaa, Katibu huyo alisema soko la kuuza dhahabu limekuwa ni tatizo kubwa kwa wachimbaji wadogo, wengi wamekuwa wakiuza dhahabu yao kwa bei ya hasara kutokana na kukosa taarifa za viwango vya uuzaji wa dhahabu na hii inawafanya kila mmoja kuuza kwa bei yake na kuwanufaisha zaidi wanunuzi.

Hata hivyo, Katibu Hatari Bwatwa alisema mbali na changamoto hizo zinazogusa shughuli zao za uchimbaji, wanakabiliwa na hatari ya kuibuka kwa magonjwa yanayochangiwa na muingiliano wa watu, hivyo akaomba serikali iwasaidie kutoa elimu kwa wachimbaji hao na watu wanaoishi jirani na mgodi.

“Wachimbaji wadogo wa dhahabu ni wengi na sehemu kama hizi za machimbo suala zima la maadili lipo chini, maana ni sehemu ya mkusanyiko na watu wanaotoka sehemu mbali mbali, hivyo magonjwa ya zinaa yanashamiri, watoto kuacha shule, vitendo vya ubakaji, mabinti kujiuza, hivyo wakati serikali ikishughulikia namna ya kutatua changamoto za wachimbaji, kwa upande wa pili itengeneze mazingira rafiki yatakayo rekebisha maadili hasa sehemu hizi za migodi” alisema.