MVUA YAHARIBU NYUMBA, MAZAO NA MIUNDO MBINU MUSOMA VIJIJINI

Diwani wa Kata ya Bukima January Simula (wa pili kutoka kulia) akiwa na Mtendaji wa Kata ya Bukima (wa pili kutoka kushoto) na Mtendaji wa kata ya Katata Charles Buremo (wa kwanza kutoka kushoto) wakiwa kwenye ziara ya kutembelea waathirika wa mvua.

Na. Fedson Masawa

MVUA kubwa iliyodumu kwa takribani masaa sita imesababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu mbalimbali katika vijiji vya kata ya Bukima.

Mvua hiyo iliyonyesha 7, Novemba mwaka huu ilianza kunyesha asubuhi hadi mchana imesababisha familia nyingi kukosa makazi baada ya nyumba zao kubomoka na nyingine kupata nyufa.

Aidha, mvua hizo zimesababisha vyoo vya shule ya sekondari Bukima kutitia, mazao kusombwa na maji pamoja na barabara kukatika.

Mtendaji wa kata ya Bukima Peter Magesa alisema, kijiji cha Kastam ndicho kilichokumbwa na mafuriko zaidi kwani maji yalivamia kaya mbalimbali.

Hata hivyo Magesa alifafanua kuwa, kijiji cha Butata na Bukima, waathirika wake ni wa nyumba kubomoka wala siyo kujaa maji kama ilivyo Kastam.

“Wakulima wengi katika kijiji cha Kastam wameharibikiwa na mazao yao kama vile mihogo, mahindi na viazi kwani mashamba yao yamefunikwa na maji” alisema Magesa.

Magesa aliendelea: “mvua hiyo pia imeharibu miundo mbinu ya barabara hasa katika daraja ya Nyegugu, Kurumonyo (mpakani mwa Butata na Bukima) pamoja na daraja kubwa ya Bukima (barabara ya kuelekea Busekera) jambo lililosababisha huduma ya usafiri kufungwa kwa muda.”

Akizungumzia idadi ya kaya zilizoathirika na mvua hizo, Magesa alisema, ndio kwanza serikali za vijiji na kata zinapita kuchukua orodha baadaye itatolewa takwimu iliyo sahihi.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Bukima January Simula aliwapa pole waathirika wote kwa tukio lililowapata na kutoa agizo kwa mtendaji wa kata ya Bukima awaandikie barua watendaji wote wa vijiji vya kata hiyo ili kuwapa barua wananchi wanaoishi kwenye maeneo hatarishi wahame mapema na hata wale ambao nyumba zao zimeonesha dalili za nyufa wachukue tahadhari na kupisha nyumba hizo haraka sana.