WANANCHI WA KIJIJI CHA CHITARE WAANZA UJENZI WA SHULE MPYA

Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Chitare wakishiriki katika shughuli za ujenzi wa shule mpya inayoendelea kujengwa katika kitongoji cha Mwikoko.

 Na. Mwandishi Wetu

WANANCHI wa kijiji cha Chitare kwa kushirikiana na serikali ya kijiji hicho wameanza ujenzi wa shule mpya ya msingi katika kitongoji cha Mwikoko kilichopo kijijini hapo.

Hamasa hiyo inatokana na makubaliano baina ya wananchi wa Chitare na serikali yao kwa kuzingatia kigezo cha umbali wanaosafiri watoto kutoka vitongoji vya Kasia na Mwikoko hadi kitongoji cha Kumsima ilipo shule ya Msingi Chitare A na B.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Mwenyekiti wa kijiji cha Chitare Zakayo Mbogora alisema, jiografia ya kijiji cha Chitare ni kubwa, lakini pamoja na kuwepo kwa shule mbili za Chitare A na B ambazo zimeungana pamoja, bado muundo huo hauwapunguzii umbali watoto wanaotokea vitongoji vya Kasia na Mwikoko, hivyo serikali ya kijiji na wananchi wamelazimika kujenga shule nyingine itakayokuwa karibu na vitongoji hivyo.

Mwenyekiti alisema, wameamua kuanza na ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na ofisi moja ya walimu, lakini malengo yao ni kufikisha idadi ya vyumba 10 vya madarasa pamoja na ofisi tano za walimu.

“Jiografia ya Chitare ni kubwa, tunazo shule mbili A na B, lakini shule hizi zipo pamoja. Sasa muundo huu bado unaleta shida kwani watoto wetu wanaendelea kusafiri umbali mrefu kutoka Kasia na Mwikoko hadi kitongoji cha Kumusima. Pia tumeamua kuanza na vyumba viwili na ofisi na tunalenga kufikisha vyumba kumi na ofisi tano” alisema mwenyekiti huyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi wa kijiji cha Chitare wamesema, wameamua kuchangia shughuli za ujenzi wa shule mpya na tayari wameanza kujenga, lakini bado wanahitaji mchango mkubwa kutoka kwa Mbunge wao Prof. Sospeter Muhongo na serikali kwa ujumla ili kufanikisha malengo yao na kuwaokoa watoto wanaoendelea kuumia na umbali kufuata elimu.

Kwa upande wake msaidizi wa Mbunge Fedson Masawa, aliwashukuru wananchi wa kijiji cha Chitare na serikali yao kwa maamuzi mazuri waliyoyafikia na kuongeza kuwa, kama maamuzi hayo yangefanyika mapema basi leo kijiji cha Chitare wangekuwa wamefikia hatua nzuri kwani mpango huo aliuzungumza kwenye mikutano na vikao alivyowahi kufanya kijijini hapo.

Fedson alishauri serikali ya kijiji cha Chitare kukaa pamoja na kamati za shule ya Chitare A na B na kukubaliana ili michango yote inayoletwa kijijini hapo kwa ajili ya ujenzi, ielekezwe kwenye shule hiyo mpya kwani madarasa 14 ambayo yatabakia shuleni hapo yatakuwa yamekidhi uhitaji.

Alisema, bado yapo matofali yaliyotokana na saruji aliyotoa Prof. Muhongo na kama wakikubaliana matofali hayo yajenge shule mpya huku akisisitiza kuwa Mbunge yupo pamoja nao katika ujenzi huo wa shule mpya na shule zote za Jimbo lake.

“Ndugu zangu niwashukuru kwa jitihada mlizozifikia, ni maamuzi mazuri na kama mngeyazingatia toka mwanzo basi leo tungekuwa mbali. Mbunge yupo pamoja nanyi katika ujenzi wa shule hii mpya, ninachowashauri serikali ya Chitare ni kwenda kukaa na kamati ya Chitare A na B ili nguvu kubwa sasa tuielekeze katika kujenga shule hii mpya” alisema na kushauri msaidizi huyo.