KIJIJI CHA BUKIMA WATEKELEZA MAAGIZO YA WARD C, WAANZA UJENZI

Mafundi wakiendelea na ujenzi wa shule ya msingi Majita B.

Na. Fedson Masawa

VIONGOZI wa serikali ya kijiji cha Bukima kwa kushirikiana na wananchi wa kijiji hicho wameanza kutekeleza maagizo ya Ward C ya kufanikisha mahitaji ya wananchi katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya elimu hasa ujenzi wa vyumba vya madarasa.

Hatua hiyo ya utekelezaji imefikiwa siku chache baada ya kikao cha Ward C Bukima kuagiza viongozi wa serikali ya kijiji cha Bukima kuanza haraka ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Majita “B”.

Kijiji cha Bukima kwa sasa kimeanza ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na ofisi moja ya walimu ukiwa ni mpango wa ujenzi wa vyumba saba vya madarasa katika shule mpya ya Majita “B”.

Ujenzi huo wa vyumba vya madarasa unafadhiliwa na Mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo ambaye anachangia saruji ili kufanikisha ujenzi huo.

Kwa awamu ya kwanza, Mbunge huyo amechangia mifuko 60 ya saruji ambayo imefyatua matofali kwa ajili ya ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Bukima Murungu Murungu amefafanua kuwa, baada ya serikali kukubaliana kuihamisha shule B, zoezi la ujenzi limeanza kwa kasi na wanatarajia kukamilisha ujenzi wa vyumba hivyo viwili ndani ya mwezi huu wa Septemba au mwanzoni mwa mwezi Oktoba.

Murungu amekiri kwamba serikali yake ilifanya makosa mwanzoni, lakini hatarajii makosa hayo yajirudie tena kwani ujenzi wa vyumba 7 vya madarasa siyo kazi rahisi na bila kuendana na kasi ya Mbunge wao yeye na serikali yake wanaweza kuchukua miaka mingi bila kufanikisha mahitaji hayo.

“Serikali yangu imefanya makosa hapo nyuma, lakini kamwe sitarajii wala sitavumilia makosa hayo yajirudie. Tuna mzigo mzito wa ujenzi wa vyumba 7, lakini bila kuungana na Mbunge wetu na kasi yake mimi na serikali yangu hatutaweza kwa kipindi hiki kifupi” amekiri na kueleza Murungu.

Akizungumza kwa njia ya simu Diwani wa kata ya Bukima January Simula alisema, jitihada za wananchi na viongozi wa Bukima kwa sasa zimeonekana, lakini kuna saruji mifuko 60 iliyotolewa na Prof. Muhongo imebakia ambayo viongozi wa Butata wanatakiwa wakamilishe upigaji lipu vyumba vyao vya madarasa walivyovijenga.

“Kama watashindwa kukamilisha kazi hiyo ndani ya siku 10, mifuko hiyo tutaihamisha na kuwapelekea Bukima ili iwaongezee nguvu” alisema Simula.

Naye msimamizi wa shughuli za ujenzi huo Mnubi Mahindi ambaye pia ni mjumbe wa serikali ya kijiji cha Bukima alisema, serikali yao tayari imeweka pembeni tofauti zao kwa sasa wanafanya kazi kwa pamoja kwani wanacho kibarua kigumu cha ujenzi wa vyumba 7 vya madarasa.

“Hatuna tofauti yoyote kwa sasa, kazi tuliyo nayo ni ujenzi wa vyumba 7 vya madarasa, hiki ni kibarua kigumu ni muhimu sasa kuungana na Mbunge ili tufanikishe kutatua changamoto za elimu katika shule zetu” alisema Mahindi.