NGUVU KAZI WAKABIDHIWA MASHINE YA UMWAGILIAJI

Kikundi cha nguvu kazi kutoka kijiji cha Nyabaengere wakikabidhiwa mashine ya umwagiliaji na diwani wa kata ya Musanja Elias Ndaro (mwenye fulana ya kijani na njano) na Afisa kilimo kata Majura mfungo (wa kwanza kulia) Masatu Manyama, kwaajili ya kuongeza ufanisi katika kilimo chao na kuacha kutegemea mvua ambazo hazina uhakika.

Na. Verdiana Mgoma

UONGOZI wa kikundi cha Nguvu Kazi kilichopo kijiji cha Nyabaengere kata ya Musanja, umekabidhiwa mashine ya umwagiliaji kwaajili ya kuongeza tija ya kilimo chao.

Makabidhiano hayo yamefanyika kwenye shamba la kikundi hicho na kuongozwa na diwani wa kata ya Musanja Elias Ndaro, Afisa Kilimo wa kijiji cha Nyabaengere Majura Mfungo na baadhi ya wanachama wa kikundi hicho akiwemo Kiongozi wao Masatu Manyama.

Akizungumza mara baada ya makabidhiano hayo, Majura Mfungo alisema, watu wengi wanashindwa kuanza kilimo cha umwagiliaji kwa kukosa mtaji wa kununua vifaa na hata ambao wanaendelea na kilimo hicho kwa kutumia ndoo, hawapati mavuno bora.

“Hizi ni baadhi ya changamoto zinazotokea katika jamii zetu hasa kwenye upande wa kilimo cha umwagiliaji, sisi viongozi tumeamua kuunga mkono sera ya kuinua kilimo hicho cha umwagiliaji na kuna mambo tunayozingatia kwenye uhamasishaji ikiwa ni pamoja na kuendelea kuhamasisha watu kujitokeza kwa wingi kwenye kilimo hiki” alisema Mfungo.

Afisa Kilimo huyo aliongeza: “pia tunahamasisha matumizi bora ya maji katika kilimo, maendeleo yatakayoonekana kwenye kilimo cha umwagiliaji kiuchumi, kijamii na kimazingira na zaidi kilimo hicho cha umwagiliaji kuwa endelevu”

Kwa upande wake diwani Elias Ndaro alifafanua kuwa, mashine hiyo ni mwendelezo wa matumizi sahihi ya fedha za mfuko wa jimbo ambapo mwaka jana Mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo alizindua mpango huo kwa kukabidhi mashine za umwagiliaji kwa vikundi 15.

“Maamuzi tuliyofikia ni kwamba, kwenye kata yetu kila baada ya mwaka na nusu mashine ya umwagiliaji inahamishiwa kijiji kingine kwa malengo kuwa kata nzima wanufaike na mashine hiyo” alisema diwani Ndaro.

Diwani Ndaro alisema, ili kupata maendeleo na fursa mbalimbali vikundi vilivyopo ndani ya kata yake vinapaswa kujisajili na kuandaa katiba na kufungua akaunti benki ambayo itawasaidia kuhifadhi fedha zao.

“Tunamshukuru sana mbunge wetu kwa msaada huu mpaka sasa vijana wengi wamejikita zaidi katika kilimo” alisema diwani huyo.

Kwa upande wake kiongozi wa kikundi cha Nguvu Kazi Masatu Manyama aliwashukuru viongozi mbalimbali wanaowaunga mkono katika shughuli zao za kilimo hali ambayo inawafanya wazidi kuongeza juhudi.

Manyama alisema, viongozi wao wamekuwa msaada mkubwa katika kukabili changamoto wanazokutana nazo hasa kwa upande wa kilimo, lakini zinatatuliwa na kuwafanya wasonge mbele zaidi.

Kiongozi huyo alisema, awali kabla ya kukabidhiwa mashine hiyo, walikuwa wanatumia mashine ya kukanyaga kwa mguu na wakati mwingine walikuwa wanamwagilia kwa kutumia mikono, lakini sasa watakuwa wakulima bora baada ya kupata mashine hiyo.