SERIKALI YA KIJIJI CHA BUKUMI YAKUBALIANA KUCHANGIA MFUKO WA MAENDELEO

Mtendaji wa kijiji cha Bukumi Alfred Onyango akisoma ajenda za kikao cha kujadili maendeleo ya kijiji hicho, kulia kwake (mwenye kofia) ni Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji cha Bukumi Nyaonge Masatu na anayefuatia ni Mtendaji wa Kata ya Bukumi Leftinant Mkama. 

Na. Fedson Masawa

SERIKALI ya kijiji cha Bukumi imekubaliana kuchangia fedha kwa ajili ya mfuko wa maendeleo kwa shule za msingi na sekondari.

Mtendaji wa Kijiji cha Bukumi Alfred Onyango akizungumza kwenye kikao maalum cha kujadili mfuko wa maendeleo alisema, shughuli za utekelezaji wa maendeleo ya ujenzi yanaenda vizuri kwani tayari chumba kimoja cha darasa katika shule ya msingi Bukumi kimekamilika na katika ujenzi huo, mifuko mitano ya saruji imebaki huku vyumba vyote vikiwa vimepigwa lipu nje na ndani.

“Katika shule ya msingi Burungu utekelezaji wa shughuli za maendeleo unaendelea, ukamilishaji wa kupiga lipu ndani na nje pamoja na sakafu umefikia hatua nzuri na saruji iliyopo itakamilisha kabisa chumba hicho” alisema Onyango.

Aidha, wakichangia kipengele cha agizo la Mkuu wa Wilaya, wajumbe wa serikali ya kijiji cha Bukumi wakiongozwa na Koporo Chirongo alisema, Mkuu wa wilaya ni kama amewatangulia kwa kuwa michango hiyo tayari kijiji cha Bukumi wanayo na wanaendelea nayo hadi hapo watakapofikia hatua ya kumaliza uhaba wa madarasa na maabara katika kijiji na kata yao.

Hata hivyo, akiweka msisitizo kwenye hoja hiyo, Mwenyekiti wa kitongoji cha Burungu na mjumbe katika serikali ya kijiji cha Bukumi Bahati Tengule alisema, suala la mtoto kupata elimu bora si la kufikiria, ni kitu cha kukubaliana na agizo na hata kama asingesema Mkuu wa Wilaya, bado wazazi na viongozi wanatakiwa kuwajibika.

Tengule alisema, wanachohitaji ni kuona watoto wanafaulu masomo ya Sayansi siyo kuendeleza changamoto za Sayansi kama walizoziacha shuleni hapo ikizingatiwa masomo hayo ndio yenye ajira ya uhakika.

“Nimesoma kwenye shule ile na kero ya maabara naijua sana. Na leo bila kusoma masomo ya Sayansi, utajiriwaje? Sisi ni wazazi tukubaliane twende kwenye utekelezaji” alisema Tengule.

Kwa upande wake mmoja wa wajumbe kwenye kikao hicho Mangerepa Misana aliibua wasiwasi wa mchango wa maabara wa shilingi 5,000 na kusema fedha kama hizo zilichangwa na mrejesho wa matumizi yake haujawahi kurudishwa tangu mwaka 2014 yapata takribani minne.

Mangerepa aliomba kama kuna uwezekano mtendaji aliyehusika kukusanya michango hiyo arudishwe Bukumi awasomee wananchi taarifa ya mapato na matumizi ili roho zao zirudi pamoja na waendelee na mchango mwingine kama alivyoagiza Mkuu wa Wilaya.