KIJIJI CHA CHIRORWE WAOMBA MSAADA WA KUMALIZIA JENGO LA ZAHANATI

Mafundi wakiwa katika zoezi la uezekaji wa jengo la zahanati ya kijiji cha Chirorwe kata ya Suguti

Na. Verdiana Mgoma

KAMATI ya afya Halmashauri ya Musoma vijijini kwa kushirikiana na wananchi wa kijiji cha Chirorwe, wamekusudia kuboresha huduma ya afya kwa kukamilisha jengo litakalotumika kwa ajili ya zahanati ya kijiji hicho.

Mwenyekiti wa kijiji cha Chirorwe Maingu Msai, alisema wameamua kujitolea katika ujenzi wa zahanati hiyo ili kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa huduma za afya inayowakabili kwa muda mrefu.

Mwenyekiti huyo alisema, wananchi wameamua kuchangia nguvu kazi hadi hatua waliyofikia, na hatua iliyobaki wameomba msaada kwa serikali na wadau mbalimbali ili waweze kumalizia.

“Tuliomba msaada serikalini tukafanikiwa kupaua, tulipokea milioni 30, lakini bado tunahitaji msaada mkubwa ili kukamilisha jengo hili kwa kuwa lengo letu ni kuwepo na huduma ya afya kijijini hapa” alisisitiza Msai.

Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho Nyakwesi Masatu, akizungumza na mwandishi wa habari hizi kijijini hapo alisema, moja ya changamoto kubwa wanayokumbana nayo hasa akina mama, ni umbali wa kufuata huduma ya afya.

Nyakwesi alisema, kijijini kwao huduma ya afya ya uzazi wa mama na mtoto ambazo ni upimaji wa mama wajawazito na watoto, kuzalisha na kufatilia makuzi ya watoto, hazipatikani, hivyo husababisha akinamama kupoteza maisha au kiumbe kinachozaliwa.

Alisema, akinamama pia kwa kukosa huduma za karibu wanapata magonjwa mengine kama fistula, ikizingatiwa kijiji chao hakina gari la kubebea wagonjwa.

“Hatuna usafiri ambao unaweza kutufikisha kituoni kwa wakati, watoto wanaozaliwa kukosa huduma za afya kama chanjo na ukuaji wa shida, ombi langu kwa serikali tuweze kupata msaada wa mahitaji yetu na kukamilika kwa jengo hili utasaidia, maana sehemu tunapofuata huduma ni kijiji cha jirani kutoka tunapoishi” alisema Nyakwesi.

Kwa upande wake Mtendaji wa Kata ya Suguti Danford Gaudance alisema, kata hiyo pekee ndio ambayo haina zahanati, hivyo inawapa wakati mgumu wakazi wa kijiji hicho kufuata huduma ilipo.

Afisa Mtendaji huyo alisema, nia yao ni kusogeza huduma karibu na walengwa hasa akina mama wajawazito, watoto na wazee, lakini bado wanahitaji msaada mkubwa ili kukamilisha jengo hilo.

Miongoni mwa msaada wanaohitaji ni saruji, milango, madirisha na vifaa vya hospitali, huku akifafanua kuwa, fedha walizopokea ni kwa ajili ya kuezeka tu, hivyo mahitaji bado ni mengi na lengo lao ni kuondoa adha ya wakazi wa kijiji hicho kuwa mbali na huduma ya afya.