KATA YA BUSAMBARA YATAJWA KUWA MFANO WA KUIGWA KWENYE KILIMO

Afisa kilimo wa kata ya Busambara, Benard Otieno (kulia) akitoa maelekezo kwa Mwalimu Magreth katika moja ya mashamba darasa ya zao la mtama.

Na. Mwandishi Wetu

IMEBAINIKA kata ya Busambara ni miongoni mwa Kata zilizofanya vizuri katika kilimo cha mazao ya alizeti, mtama na Mihogo kutokana na wakulima wa vijiji vilivyopo kwenye kata hiyo kufuata maelekezo ya kitaalamu na kulima kisasa.

Hali hiyo imedhihirika hivi karibuni wakati wa ziara ya Msaidizi wa Mbunge la Jimbo la Musoma vijijini, Ramadhan Juma wakati akikagua mashamba darasa ya mazao ya mtama na mihogo katika kijiji cha Kwikuba, Mwiringo na Maneke..

Akizungumza kwa niaba ya wakulima wakati wa ziara hiyo, afisa kilimo wa kata ya Busambara Benard Otieno alisema, baada ya kupokea msaada wa mbegu hizo kutoka kwa Mbunge, aliitisha vikao katika vijiji vyote vitatu vya kata ya Busambara na kuwahimiza wananchi kulima mazao hayo kwa kuzingatia kanuni za kilimo bora.

“Niliwagawia wananchi mbegu za alizeti kwa maana zilikuwa nyingi sana, mbegu za mihogo na mtama zilikuwa chache, hivyo tulikubaliana na wananchi kuwa zielekezwe kwenye taasisi na kwa baadhi ya wakulima mashuhuri na tukafanikiwa. Hakika najivunia mafanikio ya kilimo katika Kata yangu, tuna zaidi ya heka thelathini za alizeti, hekakumi na moja za mtama na heka nane za mihogo. Heka za mtama na mihogo ni kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu za baadae, yaani ni mashamba darasa” alisema Otieno.

Aidha, afisa kilimo huyo alimshukuru Mtendaji wa Kata hiyo Victor Kasyupa kwa kuleta chachu ya kilimo cha alizeti baada ya kuamua kulima heka mbili kama shamba la mfano.

“Shamba lake limestawi vizuri sana kwa maana alifuata ushauri wa wataalamu wa kilimo, hakika atapata mavuno mengi” alisisitiza Otieno.

Pamoja na mafanikio hayo, afisa kilimo huyo alisema zipo changamoto zilizowakabili baadhi ya wakulima wa alizeti ikiwemo upungufu wa mvua, hali iliyosababisha baadhi ya mazao kukauka.

Hata hivyo, Afisa kilimo huyo aliwatupia lawama wakulima hao kwa kuchelewa kupanda kama alivyokuwa amewaelekeza, huku akimuomba msadizi wa mbunge kufikisha ombi lao kwa Mbunge la kupata mashine ndogo ya kukamulia alizeti ili wauze mafuta badala ya kuuza alizeti ambayo haijakamuliwa.