MVUA NA UPEPO MKALI WASABABISHA UHARIBIFU WA NYUMBA 45 BUKUMI

Moja ya nyumba zilizopata madhara kutokana na upepo mkali ulioambatana na mvua na kusababisha kaya 45 kukosa makazi kwenye vijiji vitatu vya kata ya Bukumi.

Na. Fedson Masawa

MVUA kubwa iliyoambatana na upepo mkali imesababisha kaya 45 kukosa makazi katika vijiji vitatu vya kata ya Bukumi.

Majengo mengine yaliyoezuliwa katika tukio hilo lililotokea 2, Juni, majira ya usiku, ni pamoja na jengo moja la ghala la kijiji cha Bukumi pamoja na jengo la Kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) lililojengwa na kikosi hicho kijijini Busekera.

Jumla ya nyumba zilizoezuliwa kwa kila kijiji ni 10 pamoja na jengo moja la stoo ya kijiji cha Bukumi, nyumba moja katika kijiji cha Buraga na kijiji cha Busekera ni nyumba 33 na jengo moja la kikosi cha JKT.

Akitoa taarifa kwa mwandishi wa habari hizi, Mwenyekiti wa kijiji cha Bukumi Nyaonge Masatu alisema, alipata taarifa alfajiri ya 3, Juni kutoka kwa waathirika wa tukio hilo na kuagiza ipigwe ngoma ya kuwajulisha wananchi wote wasitishe shughuli zao kwa siku hiyo ili washiriki kuwapa msaada wenzao waliopatwa na matatizo hayo.

Mmoja wa waathirika wa tukio hilo, mzee Malima Maira alisema upepo ulianza kuvuma ukionekana wa kawaida, lakini ghafla ukaongezeka nayeye alishtukia paa lote la nyumba likinyanyuliwa kwa upepo huo na kutupwa mbali na nyumba yake.

“Kilichofuata ni mimi na familia yangu kuloa kwa mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha, lakini tulijitahidi kuwaondoa watoto waliokuwemo ndani ya nyumba” alisema mzee Maira.

Aidha aliongeza, mbali na mke wake ambaye aliumia kidogo kwa kupigwa na tofali, anamshukuru Mungu kwani hakuna mtu aliyeumia vibaya katika ajali hiyo, japo chakula kama unga uliokuwemo ndani wote uliharibika kwa mvua hiyo.

Naye Nyamweko Chui maarufu kwa jina la ‘Nyakajore,’ alisema tukio hilo ni mara ya kwanza kumtokea na ilikuwa usiku, hivyo hakuwa na namna yoyote ya kutoa msaada kwa familia yake iliyokuwemo ndani na kuomba msaada kwa majirani.

Alisema, mbali na mali zilizoharibika na kupotea, watoto wameumia kwa kiasi kikubwa kwani wengine walikuwa wanalaliwa na matofali na tayari wamechukuliwa na diwani wa kata ya Bukumi na kupelekwa hospitali kwa ajili ya matibabu.

“Sijawahi kutokewa wala kushudia hili linatokea, ni mara yangu ya kwanza, tena hii ni usiku sasa, hata watoto wangu siwaoni nikashindwa kabisa kutoa msaada kwao na mali zangu. Watoto wangu wamejeruhiwa, namshukuru Mungu diwani amewapeleka hospitalini” alisema Nyamweko.

Kwa upande wake Juliana Manumbu, alisema haelewi kabisa kilichotokea na anaona ni kama miujiza tu itokee ili kuirudisha nyumba yake katika hali iliyokuwepo, kwani hana kitu chochote anachokitegemea ili kufanikisha kuiezeka nyumba yake na kuishi humo tena kama awali.

Diwani wa kata ya Bukumi, John Kurwijira ameelezea kusikitishwa na tukio hilo na kuongeza kuwa tayari uongozi wa kata na vijiji wameshachukua hatua za kupeleka kwenye matibabu majeruhi pamoja na kuwaomba wananchi walioguswa na tukio hilo waweze kuchangia chochote ili waathirika wapate huduma ya chakula.

Diwani huyo alisema, tayari wananchi na wasamalia wameshajitokeza kuwasaidia makazi baadhi ya waathirika hadi watakapofanikisha makazi yao tena na kuomba msaada zaidi kutoka serikalini na wasamalia wema ili kuwasaidia waathirika hao.

“Ndugu wananchi nimalizie kwa kuwasihi mjitahidi kujenga nyumba imara na kuziezeka kwa ubora. Hii itapunguza kasi ya uezukaji wa nyumba zetu. Lakini pia tujitume kupanda miti katika makazi yetu na kuzunguka maeneo ya jirani ili kupunguza kasi ya upepo mkali” aliwasihi diwani John Kurwijira.