WANANCHI SUGUTI WAPATA MBADALA WA ZAO LA MAHINDI AMBALO LINASUASUA

Mkulima wa kijiji cha Kusenyi, Idefonce Max akiwa na kijana wake Martin wakipalilia mtama.

Na. Verediana Mgoma

BAADHI ya wananchi wa vijiji vya Kata ya Suguti wameamua kujitosa kulima zao la mtama baada ya mahindi kushindwa kustahimili ukame.

Mmoja wa wakulima hao Idefonce Max alisema, baada hali ya hewa kubadilika na kuwepo kwa mvua za kusuasua, alichukua maamuzi ya kulima mtama kwa kuhofia huenda zao la mahindi lisingeweza kustahimili mabadiliko ya msimu wa hali ya hewa.

Mkulima huyo alisema, baadhi ya wanakijiji wenzake waliolima mahindi wameshindwa kufikia malengo yao kutokana na kuwepo kwa mvua chache na wadudu walioshambulia mazao yao, hivyo imebidi yeye kuwa mfano kwa wengine kuhusu kilimo hicho cha mtama.

Mwenyekiti wa kijiji cha Kusenyi, Magesa Mashauri amekiri kuwepo kwa changamoto kwenye zao la mahindi hasa kwa wakulima waliozoea kilimo hicho, ambapo msimu uliopita hawakuweza kufanikiwa kwenye mavuno ya mahindi na kusababisha tatizo la njaa kwenye eneo lake.

“Baada ya kumueleza mbunge kuhusu suala la msaada wa chakula aliona njia pekee ni kubadilisha mazao ya chakula kuwa mtama na mihogo, haya ni mazao yanayoweza kustahimili ukame hivyo akachukua jukumu la kuendelea kuhamasisha wananchi katika kilimo hicho na baadhi wameanza kunufaika” alisema Mashauri.

Mashauri aliongeza: “mbunge hakuishia tu kuhamasisha kilimo cha mtama na mihogo, lakini pia ametoa msaada wa mbegu za mtama na mihogo ambazo zimegawanywa kwa wanakijiji na taasisi kwa dhumuni la kutunza mbegu kwa mahitaji ya kijiji kizima kwa msimu ujao”

Kwa upande wake Afisa Kilimo wa Suguti, Masinde Mjarifu alisema kuna aina ya mbegu 30 za mtama zinazolimwa kama chakula na hustawi kwenye aina zote za udongo.

“Maeneo mazuri ni udongo wa mfinyanzi, lakini pia kwenye udongo ambao una kiasi kidogo cha mchanganyiko wa kichanga na huvumilia udongo wenye chumvi kuliko mahindi, hapo nyuma watu walipenda zaidi kulima mahindi kwa sababu huleta mazao mengi kwa ekari, lakini wakati wa ukame watu hurudi kwenye mtama kwasababu huvumilia zaidi ukame” alisema Mjarifu.

Aidha, afisa kilimo huyo alitaja matumizi ya mtama; ni kwaajili ya kupikia uji, mikate na pombe, lakini pia majani na mabua ya mtama hutumika kama lishe ya mifugo na matumizi mengine ni kutandikia paa ya nyumba.

“Nilipokea jumla ya kilo 50 ya mbegu za mtama na magunia 42 ya vipando vya mihogo kutoka ofisi ya mbunge, mbegu hizi nimezigawa kwa usawa kabisa kwenye vijiji vinne kwa wananchi, vikundi na taasisi ambazo hao waliopata ndio watakaotupatia mbegu kwa msimu unaofuata hivyo shukrani za pekee zimwendee mbunge wetu na mpaka sasa mabadiliko katika sekta ya kilimo yanaonekana” alimaliza Masinde Mjarifu.