MADAKTARI BINGWA KUTOKA CHINA WATOA HUDUMA ZA AFYA MUSOMA VIJIJINI

Baadhi ya wananchi wa Kata ya Nyambono wakisubiri kupata huduma ya afya na matibabu kutoka kwa madaktari bingwa kutoka China.

Na. Mwandishi Wetu

MBUNGE jimbo la Musoma na Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo, kwa mara nyingine ameleta timu ya madaktari bingwa kutoka China kwa ajili ya kutoa matibabu katika Zahanati mbalimbali za Jimbo hilo.

Huduma hiyo ya matibabu ilianza kwenye kata ya Nyambono na kuendelea kwenye kata ya Kwikuba ambapo wananchi walijitokeza kwa wingi kupima afya zao na kupatiwa matibabu.

Akizungumza kabla ya kuanza zoezi hilo kwenye zahanati ya Nyambono, Prof. Muhongo alisema, matibabu hayo yanatolewa bure ambapo mbali na vipimo, wananchi watakaogundulika wanasumbuliwa na magonjwa mbalimbali, watapatiwa dawa bila malipo yoyote.

“Hapa Nyambono madaktari wapo kwa siku mbili, nadhani kwa hizi siku mbili wagonjwa wa maeneo haya watapata matibabu, na ndugu zetu hawa wachina hamlipii chochote, ni kwamba wagonjwa mtapata matibabu bure, isitoshe watawapatia dawa” alisema Prof. Muhongo.

Aidha, madaktari hao wametunukiwa vyeti vya kutambua mchango wao kwa jimbo hilo; tayari wameshatoa huduma hiyo kwenye kata ya Murangi, Mugango na Nyasusura.

Wakati huo huo katika jitihada za kuboresha huduma za afya, Prof. Muhongo alisema gari jipya la wagonjwa litafika jimboni na hivyo kufikisha jumla ya magari sita ya wagonjwa.

Hii ni baada ya gari moja kubwa kutoka Japan kupelekwa kituo cha afya cha Murangi na mengine manne kupelekwa katika zahanati za Mugango, Masinono na Nyasurula na Kurugee.

Prof. Muhongo aliwahimiza wananchi na viongozi kuwa makini na wasimamizi wazuri wa magari ya wagonjwa yanayoletwa jimboni ili baadaye kila zahanati ya Musoma ipate gari ya kubebea wagonjwa.

“Nanyi ndugu zangu wananchi na hata viongozi kuweni wakali sana kwenye haya magari na wale madereva wazembe wawajibishwe. Tunataka baadae kila zahanati ya jimbo letu ipate gari lake la wagonjwa endapo mtaendelea kuzitunza vizuri hizi zinazoletwa” alisema Prof. Muhongo.

Diwani wa kata ya Nyambono Mkoyongi Masatu, akizungumza kwa niaba ya wananchi wa kata ya Nyambono na Musoma vijijini, ameshukuru ujio wa madaktari bingwa kutoka China kwa ajili ya kutoa matibabu katika kata yake na kuahidi kutoa ushirikiano na kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo kwa utaratibu unaofaa katika kata yake.