MBUNGE ATOA MBEGU ZA MIHOGO NA MTAMA KWA WAKULIMA JIMBONI

Untitled

Wananchi wa Kata ya Nyegina wakikabidhiwa mbegu za mihogo na mtama kwa ajili ya kuanzisha shughuli za uzalishaji wa mbegu hizo.

Na Mwandishi wetu.

MBUNGE wa jimbo la Musoma vijijini na Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo, ametoa mbegu za mtama na mihongo kwa wananchi wa jimbo hilo ikiwa ni hatua muhimu ya kupambana na tatizo la njaa.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo la ugawaji wa mbegu lililofanyika kwenye kijiji cha Nyegina, msaidizi wa Mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini Ramadhani Juma alisema, hatua hiyo ya ununuzi wa mbegu ilichukuliwa baada ya Prof. Muhongo kupokea taarifa kutoka kwa wananchi wake waliohitaji msaada wa mbegu bora za mihogo na mtama.

“Kuna baadhi ya wananchi walimuomba mheshimiwa mbegu za mihogo na baadhi wakawa wamemuomba mbegu za mtama na mihogo. Prof. Muhongo aliagiza taarifa ya mahitaji ambapo Halmashauri wakawa wanahitaji gunia 700 ambazo ziligharimu Milioni 14. Baada ya kupokea taarifa hiyo tulienda kuwalipa Magereza Kiabakari Milioni 7 awamu ya kwanza ambayo sasa imeleta magunia 350 na ndio sasa yanasambazwa” alisema Juma.

Aidha, akizungumzia mbegu za mtama, msaidizi huyo alisema mbunge alitoa Milioni 1.2 ambazo zimetumika kununulia kilo 900 za mtama ambazo zitasambazwa  kwa wakulima.

“Kuhusu mbegu za mtama, kuanzia jana nimezigawa Majita, lakini pia tuna wasiwasi kwamba hizi mbegu za mtama, tutakapokuwa tunazigawa kuna wananchi wetu wataenda kusaga unga. Kwa hiyo tupate utaratibu, zile kaya zitakazochukua mtama ziandikwe na kwa kushirikiana hata na uongozi wa kijiji, wawe wanaenda kuwatembelea ili kujiridhisha kama kweli walipanda. Kwa hiyo niwaombe tuzitumie kama mbegu ili baadaye tupate mbegu nyingi zaidi” alisema Ramadhani Juma.

Kwa upande wake diwani wa kata ya Nyegina Majira Mchele amewataka vijana wajitokeze kushiriki kikamilifu katika kufanya shughuli za kilimo mashambani kwa ajili ya kuzalisha kwa matumizi ya baadaye siyo kuwaachia wanawake huku wao wakizurura mitaani.

“Mimi naomba vijana twendeni mashambani. Ukienda saa 12 saa 3 umetoka utaendelea na majukumu yako ili tumvushe yule mama anayeenda shambani mwenyewe. Hii mvua ni ya kukimbizana nayo, tujitume” alisisitiza diwani Mchele.

Naye Kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Musoma, Paul Makuli ambaye pia ni Afisa Kilimo wa wilaya alieleza utaratibu wa mgawanyo wa mbegu hizo kuwa zitapandwa katika ekari 87.5 kwa halmashauri nzima ambapo vikundi 9, taasisi 17 na kaya 100 zitapewa mbegu.

Akizungumza na wananchi wa Nyegina katika uzinduzi huo, Vicky Mbunde ambaye ni Kaimu mkuu wa Wilaya alimpongeza Mbunge wa jimbo la Musoma vijijini kwa juhudi kubwa anazozifanya ndani ya jimbo hilo huku akikemea tabia ya wafugaji wanaoingiza mifugo kwenye mashamba yaliyolimwa.

“Wale ambao mnafuga mifugo hakikisheni mifugo yenu mnaitengea maeneo ambayo hayajalimwa ili angalau tunayoyafanya hapa yaonekane yana faida, atakayekiuka utaratibu huu, basi sheria ichukue mkondo wake dhidi yao” alisema.

Pia Kaimu mkuu wa wilaya ametoa onyo kali kwa vijana wanaojihusisha na matendo ya ulevi huku wakishindwa kushiriki kikamilifu katika uzalishaji na kuwataka kila mmoja ashiriki kikamilifu katika uzalishaji.

“Najua mtu hawezi kwenda kulima akiwa ametumia dawa za kulevya au ametumia kilevi chochote, najua sasa hivi serikali inapambana vikali katika kudhibiti dawa za kulevya. Sasa wenye vilabu, vilabu vyote fungua kuanzia saa 9:30 jioni. Ukifungua kuanzia saa 4 au saa 5 asubuhi, mtendaji wa kata inabidi uwakamate na uwapeleke kwenye baraza la kata mara moja” alisema Vicky.

Akihitimisha zoezi la ugawaji wa mbegu hizo, Kaimu mkuu huyo wa wilaya amewasihi wananchi kushiriki kikamilifu kila mmoja na kila kaya kuwa na shamba lililolimwa na kupandwa.

“Ukaguzi utakuja kufanyika, kila kaya moja lazima iwe na zao la chakula, aidha ulime mtama ekari moja, ulime mahindi, viazi au mihogo. Tutafanya ukaguzi wa nyumba kwa nyumba, tutakuwa na mwenyekiti wa kijiji, mwenyekiti wa kitongoji ili kubaini kila kaya na shamba lake na tujitahidi sana kulima mazao yanayostahimili ukame na madiwani na viongozi wengine mtusaidie kuhamasisha” alisema Vicky Mbunde.