MKUU WA WILAYA AFUNGA RASMI MAFUNZO YA UTENGENEZAJI VIFAA VYA UMEME JUA

Untitled

Vijana waliohitimu mafunzo ya kutengeneza chaja za simu na taa kwa kutumia mionzi ya jua wakiwa kwenye picha ya pamoja wakati wa kufunga mafunzo hayo katika kituo cha Nyegina. Waliosimama nyuma ni Dkt. Hong-kyu Choi (aliyevaa fulana nyekundu), anayefuatia kuelekea kulia ni Mkuu wa wilaya ya Musoma Dkt. Vincent Naano Anney. Kushoto kutoka kwa Dkt. Choi ni Majira Mchele diwani wa kata ya Nyegina.

 

Na Fedson Masawa

MAFUNZO ya kutengeneza chaja za simu na taa zinazotumia mionzi ya jua yamefungwa rasmi huku vijana 97 wakihitimu mafunzo hayo ya siku 20.

Mafunzo hayo yamefungwa na Mkuu wa wilaya ya Musoma vijijini Dkt.Vincent Naano Anney katika kata ya Nyegina, ambapo yalitarajiwa kushirikisha vijana 100 kutoka jimbo la Musoma vijijini, lakini ni vijana 97 pekee wamehitimu baada ya vijana watatu kushindwa kushiriki kwa kutoa hudhuru.

Mbali na vijana hao,  viongozi mbalimbali wakiwemo Mwenyekiti wa kijiji cha Nyegina, Diwani wa kata ya Nyegina nao walipata fursa ya kuhudhuria mafunzo hayo yaliyoendeshwa na Dkt. Hong-kyu Choi kutoka Korea.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Nyafuru Magere kutoka kijiji cha Nyasulura alisema, ingependeza zaidi kama watajengewa kiwanda ili ujuzi walioupata kwa ajili ya uzalishaji na kujiajiri wenyewe.

“Mimi nampongeza Waziri na mbunge wetu Prof. Muhongo kwa kutuletea mafunzo haya, tumepata ujuzi wa kutosha na sasa tulikuwa tunaomba watujengee kiwanda ili tujiajiri. Vilevile napenda kuwasihi vijana wenzangu ambao hawajashiriki mafunzo haya, wasitegemee ajira kutoka serikalini, ajira ni wao wenyewe na ujasiliamali tunaoufanya ni ajira tosha” alisema Nyafuru na kuwasihi vijana wenzake wasipuuze fursa za kujiajiri.

Naye diwani wa kata ya Nyegina, Majira Mchele alimshukuru Dkt. Hong-kyu choi kwa kutumia muda wake mwingi kuwafundisha vijana wa Tanzania na Musoma vijijini na kumpongeza mbunge wa jimbo hilo kwa kuwa na uhusiano mzuri na Dkt. Choi na ubalozi wa Korea kwani ndiye aliyefanya vijana hao kuelekea kutimiza ndoto zao.

“Namshukuru sana Dokta Choi kwa kutumia muda wake, yeye ni mtu wa Korea, lakini ameamua kuugawa muda wake kwa ajili ya kuja kuwasaidia watanzania. Nimshukuru pia mheshimiwa mbunge kwa kufanya urafiki na Dokta mpaka akaibua hiki tunachokuja kukivuna. Bila Prof. Muhongo Dokta asingeijua Tanzania, wala Musoma vijijini na wala elimu hiyo msinge ipata” alisema diwani Majura.

Kwa upande wake Dkt. Hong-kyu alisema, vifaa anavyofundisha na kuvitengeneza ni muhimu na ni rahisi mno, hivyo vitawasaidia vijana kutengeneza ajira, kutoa elimu na kuboresha maisha ya watu na hatimaye vijana kufikia ndoto na matarajio yao ya usoni.

Aidha, Dkt. Choi alimshukuru Mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo kwani alipokutana naye kwa mara ya kwanza ofisini kwake akiwa na vifaa hivyo, mbunge huyo alivutiwa navyo na kumuomba  akawafundishe vijana wake 100 jimboni.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Vincent Naano Anney, aliwashukuru  wasaidizi wa Mbunge kwa kazi nzuri wanayoifanya kwa kuwaunganisha wananchi ndani ya jimbo hilo na hivyo kuharakisha maendeleo.

“Kwanza nawashukuru sana wasaidizi wa mbunge kwa kuweza kuwaunganisha wananchi wa Musoma. Hii ni kwa sababu nimejifunza kitu kutoka kwa Prof. Muhongo kwa kuweka watu wake katika maeneo yote ndani ya jimbo, nikimaanisha Nyegina, Mugango, Murangi, Saragana na Busekera. Hii inaleta mpangilio mzuri sana. Nawashukuruni sana” alisema Dkt. Naano.

Aidha, akizungumzia mafunzo hayo, Mkuu huyo wa wilaya, aliwataka vijana hao kutumia ujuzi walioupata kujitanua kifkra na kujiona kuwa wana uwezo wa kufanya mambo makubwa zaidi iwapo watakabidhiwa vifaa vya kufanyia kazi na kusambaza elimu kwa vijana wenzao.

Dkt. Naano pia alipendekeza uundwaji wa vikundi vinavyotambulika kwa ajili ya kujiweka katika hatua nzuri ya kupata misaada kutoka serikalini ikiwemo Halmashauri ya Musoma.

“Maarifa na ujuzi mlioupata wa kutengeneza hizi sola ndogo, sasa mna uwezo wa kutengeneza sola kubwa endapo mkipata vifaa. Pia nawaomba mjitahidi haya maarifa muwafundishe na wengine na mkitoka hapa mkaunde vikundi na vikundi hivi tutavifadhili kwa fedha za mfuko wetu wa halmashauri”

Mkuu wa wilaya Dkt. Vincent Naano Anney  alimalizia kwa kumshukuru Dkt. Choi pamoja na ubalozi wa Korea kwa kufanikisha kazi nzuri aliyoifanya katika jimbo la Musoma vijijini na kuahidi kuwaweka vijana katika makundi na kumthibitishia mkufunzi huyo kuwa, serikali inajipanga kupitia ubalozi wa Korea nchini ili kuhakikisha vifaa vinapatikana kwa urahisi kwa ajili ya kuwaendeleza vijana nchini.