MIRADI MINGINE YA RUWASA – KATA ZA SUGUTI NA NYAMBONO ZAKARIBIA KUANZA KUTUMIA MAJI YA ZIWA VICTORIA

MIUNDOMBINU inajengwa kwa ajili ya usambazaji wa MAJI SAFI na SALAMA (maji ya bomba) kwenye KATA za SUGUTI na NYAMBONO.

Na: Hamisa Gamba
Msaidizi wa Mbunge
Kata ya SUGUTI ina Vijiji 2 (Suguti na Kusenyi) vyenye ufukwe wa ZIWA VICTORIA, na vingine viwili (Wanyere na Chirorwe) viko mbali na Ziwa hilo.
Kata ya NYAMBONO, yenye Vijiji 2, yaani Nyambono na Saragana iko umbali wa zaidi ya kilomita 10 kutoka Ziwa Victoria.
SERIKALI imetoa Shilingi MILIONI 356  kwa Mradi wa MAJI wa Kata ya Suguti na Shilingi MILIONI 230 kwa Mradi wa  MAJI wa Kata ya Nyambono – hii ni MIRADI mingine ya RUWASA inaotekelezwa ndani ya Jimbo la Musoma Vijijini kwa Mwaka huu wa Fedha (2020/2021).
MIUNDOMBINU inajengwa kuvuta na kusambaza MAJI kutoka ZIWA VICTORIA (Kijijini Suguti) ambapo PAMPU yenye uwezo wa kusukuma LITA 67,000 kwa saa itajengwa. VIFAA vyote vimeishanunuliwa.
MAJI ya kutoka Kijijini Suguti yatasambazwa kwenye Vijiji vya Kusenyi, Chirorwe na Wanyere (Kata ya Suguti).
TENKI la ujazo wa LITA 200,000 linajengwa Kijijini Chirorwe ambapo MAJI ya Kata ya Nyambono yatachukulia kupitia Mlima Nyabherango. TENKI jingine la ujazo wa LITA 200,000 linajengwa Kijijini Saragana kwa ajili ya MAJI ya Kijiji hicho na cha Nyambono.
Kwa hiyo, RUWASA kwa sasa inakamilisha ujenzi wa MIUNDOMBINU ya kusambaza MAJI SAFI na SALAMA kwenye Kata za SUGUTI na NYAMBONO. Hapo baadae, Kata ya BUGOJI yenye Vijiji 3 (Bugoji, Kaburabura na Kanderema) nayo itafikishiwa MAJI kutoka kwenye TENKI la Kijijini Saragana.
MENEJA wa MRADI huu wa RUWASA, Injinia Mohamed Said Yamlinga amesema kuwa MIRADI ya Kata za Suguti na Nyambono itakamilika Januari 2021.
WANAVIJIJI wa Kata za SUGUTI na NYAMBONO, na VIONGOZI wao, wanaishukuru sana SERIKALI yetu kwa kutoa FEDHA za kutekeleza MIRADI ya kusambaza MAJI ya BOMBA Vijijini mwao.
Ofisi ya Mbunge
Jimbo la Musoma Vijijini