UBORESHAJI WA HUDUMA ZA AFYA VIJIJINI UNAFANYWA KWA USHIRIKIANO MZURI WA SERIKALI NA WANAVIJIJI

ujenzi unaoendelea kwenye WODI ya MAMA na MTOTO kwenye ZAHANATI ya Kijiji cha Bukima, Kata ya Bukima.

Na: Verediana Mgoma
Msaidizi wa Mbunge
ZAHANATI za Vijiji vya Jimbo la Musoma Vijijini ZAANZA kupanua ZAHANATI zao kwa kujenga WODI za MAMA na MTOTO
Jimbo la Musoma Vijijini lenye KATA 21 na VIJIJI 68 lina jumla ya ZAHANATI 28 (24 za Serikali na 4 za Binafsi). ZAHANATI MPYA 14 zinajengwa kwa ushirikiano wa SERIKALI na WANANCHI.
Jimbo hili lina VITUO vya AFYA 2 (Murangi & Mugango) na cha tatu (Bugwema) kitapatikana kabla ya Disemba 2020. SERIKALI, WANAVIJIJI na MBUNGE wa Jimbo hili, Prof Sospeter Muhongo, WAMECHANGIA ujenzi na uboreshaji wa MIUNDOMBINU kwenye VITUO hivi vya AFYA.
Jimbo hili litapata HOSPITALI ya Wilaya, yenye ufadhili mkubwa wa Serikali (Tsh bilioni 1.5), inayojengwa Kijijini Suguti, Kata ya Suguti. WANAVIJIJI na MBUNGE wao nao wanachangia ujenzi huu.
WODI ZA MAMA NA MTOTO
ZAHANATI 3 (Bukima, Nyegina na Kisiwa cha Rukuba) za Jimboni mwetu zimeanza ujenzi wa WODI za MAMA na MTOTO kwa lengo la kuboresha HUDUMA za AFYA zitolewazo kwenye Zahanati hizo.
UJENZI WA WODI YA MAMA NA MTOTO KWENYE ZAHANATI YA BUKIMA
Kata ya Bukima yenye Vijiji vitatu (Bukima, Butata na Kastam) ina Zahanati moja inayohudumia wakazi wote wa Vijiji hivyo.
WANANCHI wa Kijiji ya Bukima wameamua KUFUFUA ujenzi wa WODI ya MAMA na MTOTO uliosimama kwa takribani miaka minne. Uamuzi wa ujenzi huu ni muhimu sana kwani MAMA WAJAWAZITO wa Kijiji na Kata yote ya Bukima wanalazimika kutembea umbali ya zaidi ya kilomita 7 kwenda kupata matibabu kwenye Kituo cha Afya cha Murangi.
MTENDAJI  wa KIJIJI cha Bukima, Ndugu Josephat Phinias amesema WANAWAKE wamejitokeza kwa wingi kuchangia NGUVUKAZI zao kwenye ujenzi huu. WANAVIJIJI wanasomba mchanga, kokoto, mawe na maji.
Vilevile, Kiongozi huyo amesema, “Tumepokea RUZUKU ya Kijiji kutoka HALMASHAURI yetu, kiasi cha Tsh 6,075,000/= ambayo imesaidia kuharakisha ujenzi wetu.”
MGANGA MKUU wa Zahanati hiyo, Ndugu Malisha John ameeleza kuwa kukamilika kwa JENGO hilo kutasaidia kuboresha HUDUMA za AFYA ya UZAZI na ufuatiliaji wa MAKUZI ya WATOTO kwenye Kata hiyo na Kata za jirani zisizokuwa na huduma hizo.
DIWANI wa KATA, Mhe January Simula amesema WANANCHI wameamua kukamilisha ujenzi wa WODI hiyo na vilevile, ZAHANATI MPYA inaendelea kujengwa kwenye Kijiji cha Butata. Kwa hiyo, Kata ya Bukima yenye Vijiji 3 itakuwa na ZAHANATI 2 ifikapo Disemba 2020.
MICHANGO YA MBUNGE WA JIMBO
Prof Sospeter Muhongo, Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini AMEANZA KUCHANGIA ujenzi wa WODI ZA MAMA na MTOTO kwenye ZAHANATI zote tatu.
ZAHANATI ya Bukima imeshachangiwa SARUJI MIFUKO 100 bado mingine 100 itakayotolewa kulingana na kasi ya ujenzi huo. Mbunge huyo ameishachangia SARUJI MIFUKO 50 kwa ZAHANATI MPYA inaojengwa Kijijini Butata.
ZAHANATI ya Nyegina imeishachangiwa SARUJI MIFUKO 50, bado 150 itakayotolewa kwa utaratibu ule ule – kasi ya ujenzi.
ZAHANATI ya Kisiwa cha Rukuba imepewa SARUJI MIFUKO 50, imebaki 150. Kasi yao ya ujenzi ni kubwa.
MICHANGO YA WADAU WENGINE WA MAENDELEO
Jhpiego (Johns Hopkins Program for International Education in Gynaecology and Obstetrics,  USA) wanasaidia kutoa Huduma za Afya ya Mama na Mtoto kwa kutoa chanjo na madawa kwenye Zahanati ya Bukima na nyingine zote Jimboni mwetu.
 ICAP (International Centre for AIDS Care and Treatment Programs, USA) inatoa Huduma ya upimaji wa VVU katika jamii kwenye Zahanati ya Bukima na nyingine zote Jimboni mwetu.
AGPAHI (Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiatives, USA) inasaidia kutoa Huduma za matibabu endelevu kwa wanaoishi na VVU ndani ya Jimbo letu.
* Tunawashakuru sana WADAU hao wa MAENDELEO kwa kuendelea KUCHANGIA UBORESHAJI wa HUDUMA za AFYA Jimboni mwetu.
OMBI KUTOKA KWA WANAVIJIJI WA KATA YA BUKIMA
WANAVIJIJI wanawaomba WAZALIWA wa Kata ya Bukima washirikiane nao kwa kutoa MICHANGO ya kukamilisha WODI ya MAMA na MTOTO kwenye ZAHANATI ya Kijiji cha Bukima. Vilevile, wanaombwa wachangie ukamilishaji wa ZAHANATI MPYA inayojengwa Kijijini Butata.