SERIKALI YATOA TSH MILIONI 100 KUJENGA NYUMBA ZA WALIMU KWA KUSHIRIKIANA NA NGUVUKAZI ZA WANAVIJIJI

Ujenzi wa Nyumba 4 za Walimu kwenye Sekondari ya Tegeruka

Na: Fedson Masawa
Msaidizi wa Mbunge
UJENZI wa Nyumba nne (4) za Walimu katika Shule ya Sekondari Tegeruka iliyopo Kata ya Tegeruka umefikia hatua nzuri.
SERIKALI yetu ilitoa Tsh Milioni 100 na Wananchi wa Kata ya Tegeruka, yenye Vijiji vya Kataryo, Mayani na Tegeruka wanachangia NGUVUKAZI zao kwenye MRADI huu. Wanasomba mawe, kokoto, mchanga na maji ya ujenzi.
Nyumba mbili (2) zimeezekwa bado kupiga lipu na sakafu. Nyumba moja (1) imepauliwa tayari kwa kuezekwa na nyumba ya nne mafundi wanamimina lenta ya juu. Vyoo navyo vinajengwa.
Akizungumza na Msaidizi wa Mbunge, Mkuu wa Shule ya Sekondari Tegeruka, Mwalimu Anton Helege James alisema Sekondari yake ina uhitaji wa Nyumba 17, za Walimu, zilizopo ni 3 na inaupungufu wa Nyumba 14. Hivyo kukamilika kwa Nyumba hizo 4 kutasaidia kupunguza idadi ya Walimu wa Sekondari hiyo wanaofundisha na kuishi mbali na Shule.
WANANCHI na VIONGOZI wao wa ngazi zote hadi Wilayani na Mkoani, akiwemo Mbunge wao, WANAISHUKURU sana SERIKALI yao kwa msaada huu mkubwa wa kuanza kutatua kero ya MAKAZI ya WALIMU wa Sekondari yao.
Kuna UPUNGUFU wa Walimu wa Masomo ya Sayansi kwani kwa sasa Shule ina Walimu wa:- Physics 1, Biology 1, Chemistry 2 na Maths 2.
Mwalimu Mkuu huyo ameendelea kueleza na kusema kwamba wapo Walimu wengine 3 wa Kujitolea wa Masomo ya Sayansi – hawa wanalipwa POSHO na Wazazi wenye Watoto hapo Shuleni. Bado kuna upungufu wa Walimu wa English Geography na Maths.
Mbali ya kumshukuru Mbunge wa Jimbo kwa kuwapatia Vitabu vingi vya Masomo ya Sayansi na Kiingereza, Mwalimu Mkuu huyo amemuomba Mbunge huyo awasaidie kupata Walimu wengine wa kujitolea. Vilevile, ameomba HARAMBEE ifanyike Disemba 2019 kwa ajili ya ujenzi wa Maabara 3 za Masomo ya Sayansi. Mbunge wa Jimbo, Prof Sospeter Muhongo amekubali kushirikiana na Shule na Wananchi wa Kata ya Tegeruka kwenye ujenzi na uboreshaji wa Miundombinu ya Elimu ya Tegeruka Secondary School.