SHULE YA MSINGI MURANGI – SOMO LA STADI ZA KAZI LATUMIKA KUIMARISHA KILIMO CHA UMWAGILIAJI

Wanafunzi wa S/M Murangi iliyoko Kijijini Lyasembe wakiwa kwenye SOMO la STADI za KAZI – ndani ya Shamba la Nyanya la Shule.

Na: Verediana Mgoma
Msaidizi wa Mbunge
Shule ya Msingi Murangi iliyopo Kijiji cha Lyasembe, Kata Murangi imeamua kufanya KILIMO cha UMWAGILIAJI kupitia SOMO la STADI za KAZI.
Lengo kuu hapa ni KUWATAYARISHA WAHITIMU waweze KUJIAJIRI na KUJITEGEMEA kupitia KILIMO hasa cha UMWAGILIAJI kwani makazi yao yako karibu sana na Ziwa Viktoria.
Mwalimu Maburugi Matiko wa Shule hiyo alipata MAFUNZO ya UFUNDISHAJI wa STADI za KAZI mbalimbali zikiwemo za KILIMO. Kwa hiyo, Shule imanzisha SHAMBA DARASA la mihogo, mahindi, vitunguu, nyanya na matikiti.
MAVUNO kutoka shamba hilo yamesaidia KUKUZA UCHUMI wa SHULE. Wanafunzi wameweza kupata uji wawapo masomoni. Vilevile MATUMIZI mengine ya Shule yameboreka kutokana na mapato ya Kilimo hiki.
Mwanafunzi Samwel Manyama wa Darasa la VII Shuleni hapo, amesema kwamba anafurahia SOMO la STADI za KAZI kwa sababu analisoma kwa VITENDO na yeye mwenyewe amekuwa ANAJITOLEA kuelimisha JAMII aliyomo juu ya aina hii ya Kilimo yenye faida kubwa zaidi kuliko ile ya Kilimo kilichozoeleka cha kutegemea MVUA.
Mtendaji wa Kijiji cha Lyasembe, Ndugu Chikonya Chikonya amesema MAPATO ya Kilimo ya Shule za Msingi mbili ziliko kwenye Kijiji hicho, yamesaidia KUBORESHA baadhi ya MIUNDOMBINU ya Shule zao.
Mtendaji huyo wa Kijiji anamshukuru sana Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo kwa juhudi zake za kuboresha Sekta ya Kilimo Jimboni mwao, ikiwemo kugawa bure MBEGU za ALIZETI, MIHOGO, MTAMA na ULEZI kwa Wanavijiji (Vijiji vyote 68) na kwenye Taasisi za Elimu zinazopenda kujishughulisha na KILIMO.
Vilevile, Wakulima wa Kijiji cha Lyasembe wanamshukuru Mbunge wao wa Jimbo kwa kuwapa PAMPU/MASHINE ya UMWAGILIAJI akina MAMA wa Kikundi cha TUPENDANE cha Kijiji hicho ambacho kimeleta hamasa kubwa ya KILIMO cha UMWAGILIAJI Kijijini hapo. PAMPU/MASHINE na vifaa vyake ilinunuliwa kwa kutumia Fedha za MFUKO wa JIMBO.