SERIKALI YASAIDIA SHULE YA MSINGI KIRIBA KWENYE UJENZI WA VYUMBA VIPYA VYA MADARASA NA UPATIKANAJI WA MADAWATI

kazi za ujenzi zinazoendelea kwenye S/M Kiriba, Kijijini Kiriba – ukamilishaji wa Chumba kimoja cha Darasa na Chumba kingine ambacho hakijaezekwa

Alhamisi, 20.06.2019
Jimbo la Musoma Vijijini
Na: Fedson Masawa
Msaidizi wa Mbunge
UBORESHAJI WA MIUNDOMBINU YA ELIMU JIMBONI
TAKWIMU:
*Kata 21, Vijiji 68, Vitongoji 374
*Idadi ya SHULE za MSINGI za Serikali: 111
*Idadi ya Shule za Msingi za Binafsi: 2
*Idadi ya Shule za Msingi MPYA zinazojengwa na Wanavijiji kwa kushirikiana na Serikali: 10
*Idadi ya SEKONDARI za Kata/Serikali: 19
*Idadi ya Sekondari za Binafsi: 2
*Idadi ya Sekondari MPYA zinazojengwa na Wanavijiji kwa kushirikiana na Serikali: 7
S/M KIRIBA YAPIGWA JEKI NA SERIKALI
SERIKALI kupitia Mradi wake na Wafadhili wa EP4R imetoa jumla ya Tsh Milioni 12.5 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Chumba kimoja cha Darasa katika Shule ya Msingi Kiriba iliyopo Kijijini Kiriba, Kata ya Kiriba.
Mkuu wa Shule ya Msingi Kiriba, Mwalimu Agnes Emmanuel ameeleza kuwa, ukamilishaji wa chumba hicho kimoja umefikia hatua nzuri kwa kuzingatia maelekezo ya TAMISEMI ambayo ni pamoja na KUKAMILISHA UJENZI wa Darasa hilo na UNUNUZI wa MADAWATI 23 kwa Wanafunzi 45.
Shule ya Msingi Kiriba ina jumla ya Wanafunzi 581, inauhitaji wa Vyumba 13 vya Madarasa, vilivyopo ni 6 na pungufu ni vyumba 7. Hadi sasa jumla ya Madarasa Mawili (2) yanasomea NJE chini ya MITI.
Ujenzi wa Maboma ya Vyumba Viwili vya Madarasa ulianza Mwaka 2017 baada ya Mbunge Prof Sospeter Muhongo KUCHANGIA SARUJI MIFUKO 60 na WANAKIJIJI kuchangia NGUVUKAZI ya kusomba mawe, kokoto, mchanga na maji.
S/M Kiriba inahitaji MABATI 54 kuezekea Chumba kilichobaki cha Darasa. Mwenyekiti wa PMU wa Wilaya & Kijiji (Kiriba) Ndugu Murumba Murumba na Mtendaji wa Kijiji (VEO) Ndugu Antony Daniel Safi WAMEAHIDI kuwashawishi Wananchi wachangie MABATI 54 na kazi ya uezekaji wa Darasa lilobakia ikamilike kabla ya tarehe 30.06.2019.
Mbali ya MCHANGO huo wa Mbunge wa Jimbo, S/M Kiriba imepokea jumla ya MADAWATI 95, VITABU vya MASOMO ya Kiingereza na Sayansi kutoka kwa Mbunge wao wa Jimbo.