MKURUGENZI KAYOMBO ATOA MIKOPO YENYE THAMANI YA SHILLINGI MILLIONI 11 KWA VIKUNDI VYA KWIKUBA CARPENTRY NA AMANI NA UPENDO, HALMASHAURI YAFIKIA ASILIMIA 92.6 YA LENGO LA UTOAJI MIKOPO KWA MWAKA WA FEDHA 2018/2019*.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Ndg. John Lipesi Kayombo akikabidhi hati ya mkopo huo kwa kikundi cha wanawake kinachojulikana kwa jina la Amani na Upendo.

Alhamisi 13, June 2019
Musoma, Mara.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Ndg. John Lipesi Kayombo ametoa mikopo yenye thamani ya shillingi *11,000,000/=* kwa  vikundi 2, ambapo 1 cha vijana kinachojulikana kwa jina la Kwikuba Carpentery na 1 cha wanawake kinachojulikana kwa jina la Amani na Upendo.
Zoezi hilo la utoaji wa mikopo hiyo limefanyika leo Alhamisi 13, June 2019 katika Ofisi ya Mkurugenzi huyo iliyopo katika eneo la uwanja wa Ndege, Musoma.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya hati ya malipo ya fedha hizo Mkurugenzi Kayombo aliwataka wanufaika wa mikopo hiyo kuitumia kwa malengo yaliyokusudiwa.
“Kwa kuwajali na kuwapenda watanzania hususani wanyonge, Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dkt John Pombe Magufuli imeondoa riba kwenye mikopo ya vikundi, sasa hivi pesa utakayokopa ndio utakayorudisha” alisema Kayombo.
“Kwa hiyo nawakabidhi fedha hizi, naomba mzitumie kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuweza kurudisha mikopo hii kwa wakati na kuepukana na ucheleweshaji wa kurejesha na kupelekea kupata faini ya asilimia 10 ya kile mkichokopa” alisema Kayombo.
Sambamba na hilo Mkurugenzi Kayombo alisema Halmashauri hiyo imefikia asilimia *92.6* ya lengo la kutoa  mikopo na kubakiza asilimia *7.4* ya bajeti ya  halmashauri kwa 10% ya mikopo iliyobajetiwa.
“Bajeti ya  mapato ya ndani ya Halmashauri ya Shillingi 1,094,260,000/= kwa mwaka wa fedha 2018/2019 na kutenga asilimia 10 ya mapato hayo kwa ajili ya mikopo ya wanawake, walemavu na vijana ambayo ni Shillingi *109,426,000/=*, mpaka sasa kwa mwaka huu wa fedha tumeshatoa mikopo yenye thamani ya shillingi *101,000,000/=* kwa vikundi 25 ambayo ni sawa na asilimia *92.6* ya mikopo, imebaki asilimia 7.4 ambayo nataka mpaka ikifika 28, June 2019 fedha yote iliyobaki iwe imekopeshwa” alisema Kayombo.
“Tumetoa mikopo kwa awamu *nne* kwa vikundi 16 vya wanawake, vikundi 6 vya vijana na vikundi 3 vya walemavu, ambapo awamu  ya *kwanza tulitoa mikopo yenye thamani ya shillingi 49,000,000* kwa vikundi 6 vya wanawake, 3 vya vijana na 2 vya watu wenye ulemavu, *awamu ya pili tulitoa mikopo yenye thamaniya shillingi 20,000,000/=* kwa vikundi 4 vya wanawake, *awamu ya tatu tulitoa mikopo yenye thamani ya shillingi 21,000,000/=* kwa vikundi 3 vya wanawake, na 1 cha vijana, *pia tulitoa mkopo kutoka kwenye fedha ya marejesho shillingi 19,000,000/=* kwa vikundi 2 vya wanawake, 1 vijana na 1 cha watu wenye ulemavu, leo tunatoa mikopo kwa *awamu ya nne yenye thamani ya shillingi 11,000,000/=* kwa kikundi 1 cha wanawake na 1 cha vijana ambapo mpaka sasa tumeshatoa mikopo kwa vikundi 25” alisema Kayombo.
*Imetolewa na*
*Kitengo cha Habari na Uhusiano*
*Halmashauri ya Wilaya ya Musoma*.