KIJIJI CHA KAKISHERI CHAAMUA KUJENGA ZAHANATI YA KIJIJI CHAO

Uchimbaji (umekamilika) wa Msingi wa Zahanati ya Kijiji cha Kakisheri.

Na: Hamisa Gamba
Msaidizi wa Mbunge
Jimbo la Musoma Vijijini limechagua VIPAUMBELE 3 – ELIMU, AFYA na KILIMO. Maji, Umeme, Barabara, n.k. ni NYENZO zinazohitajika kutekeleza, kwa mafanikio makubwa, Miradi ya Vipaumbele hivyo vitatu.
Wananchi wa Kijiji cha Kakisheri, Kata ya Nyakatende, wameanza Ujenzi wa Zahanati ya Kijiji chao. Uamuzi huu unatokana na Kikao cha Wanakijiji hao na Mbunge wao Prof Sospeter Muhongo uliofanyika kwenye eneo la ujenzi mwezi uliopita (Januari 2019).
Diwani wa Kata ya Nyakatende, Mhe Rufumbo Rufumbo na Ndugu Msafiri Matete Mwenyekiti wa Kijiji cha Kakisheri wamesema kwamba LENGO LAO KUU ni kuhakikisha ujenzi wa Zahanati hiyo unakamilika na kuanza kutoa huduma za matibabu  ndani ya mwaka mmoja kuanzia mwezi huu (Februari 2019 – Februari 2020).
Ujenzi wa Zahanati hii unafuata maelekezo ya Halmashauri yao ya Wilaya ya Musoma. Kila hatua ya ujenzi inakaguliwa na Wataalamu kutoka Halmashauri yao.
Wananchi wanachanga FEDHA, wanasomba mawe, kokoto, mchanga na maji ikiwa ni MICHANGO yao kwenye Mradi huu. Wameishanunua Saruji Mifuko 50 ya kuanzia ujenzi.
Mbunge wa Jimbo, Prof Muhongo atachangia kwa kila hatua itakayafikiwa kwenye ujenzi wa Zahanati hii. Kwa hatua ya msingi (foundation) atachangia Saruji Mifuko 50 na kwa hatua ya kusimamisha Boma atachangia tena Saruji Mifuko 50.
WADAU wa MAENDELEO wanaombwa kuwaunga mkono Wananchi wa Kijiji cha Kakisheri, Kata ya Nyakatende kwenye Mradi wa ujenzi wa Zahanati yao.
“Umoja ni Ushindi, tuungane kujenga Zahanati ya Kijiji cha Kakisheri.”