UJENZI WA VYUMBA VINNE VYA MADARASA YA SHULE SHIKIZI YA MWIKOKO WAFIKIA HATUA NZURI

Moja kati ya Majengo ya Madarasa Mapya katika Shule SHIKIZI ya Mwikoko ya Kijiji cha Chitare.

Na Verediana Mgoma, Msaidizi wa Mbunge
10.11.2018
Ujenzi wa Vyumba Vinne (4) vya Madarasa na Ofisi Mbili (2) za Walimu katika Shule SHIKIZI ya Mwikoko ya Kijiji cha Chitare, Kata ya Makojo umefikia hatua nzuri ambapo Vyumba Viwili, Ofisi ya Walimu na Choo 1 vinavyojengwa kwa Mchango wa Mradi wa EQUIP (Tsh Milioni 60) vipo katika hatua ya mwisho ya ukamilishwaji. WANANCHI wanachangia NGUVU ZAO kupunguza gharama za ujenzi huu.
Kwa upande wa Vyumba Viwili (2) na Ofisi moja (1) ya Walimu vinavyojengwa kwa MICHANGO ya WANANCHI na WADAU wengine wa Maendeleo akiwemo Mbunge wa Jimbo Prof Sospeter Muhongo, vipo hatua ya ukamilishaji wa kozi mbili za mwisho.
Akizungumza na Mwandishi wa Habari hizi, Mwalimu wa Shule ya Msingi Chitare, Ndugu Charles Amon ambaye pia ni Msimamizi na Mlezi wa Shule Shikizi ya Mwikoko alisema kuwa, UMOJA wa WANANCHI wa Kijiji cha Chitare ndio umeleta mafanikio ya ukamilishaji wa shughuli hizo za ujenzi ili kuwaokoa watoto wao wanaotembea umbali mrefu kufika zilipo Shule za Chitare A na Chitare B.
Ndugu Amon aliongezea na kusema kwamba kukamilika kwa SHULE SHIKIZI hiyo  kutaboresha mahudhurio ya watoto waliokuwa hawafiki shuleni kwa ajili ya umbali mrefu wa kutembea kwenda Shule za mbali.
Aidha Mtendaji wa Kijiji cha Chitare, Ndugu Alex Masija aliwapongeza WANANCHI wa Kijiji cha Chitare katika ujenzi wa shule hiyo pamoja na WADAU mbalimbali waliowaunga mkono hadi kufikia hatua hiyo.
Ili kufanikisha ujenzi wa Shule SHIKIZI ya Mwikoko, Mbunge wa Jimbo Prof Sospeter Muhongo alichangia SARUJI MIFUKO 100. Ameridhishwa na matumizi ya Mifuko 50 ya awali na atakapokagua ujenzi huo Mwezi ujao (Disemba 2018) atatoa Mifuko 50 iliyobakia.
MAENDELEO NDANI YA VIJIJI 68 VYA JIMBO LA MUSOMA VIJIJINI YATELETWA KWA VITENDO NA SIYO KWA MANENO MATUPU – TUCHANGIE KWA VITENDO MAENDELEO YA VIJIJI VYETU!