WANANCHI WA KIJIJI CHA BUANGA KUKAMILISHA UJENZI WA SHULE JANUARI 2019

Baadhi ya Wananchi na Viongozi wakiendelea na ufyatuaji wa matofali Kijijini Buanga.

Na Verediana Mgoma, Msaidizi wa Mbunge
Oktoba 18, 2018
Wananchi wa Kijiji cha Buanga kwa kushirikiana na Viongozi wa Serikali ya Kijiji hicho wamesema wamejipanga kuhakikisha ifikapo mwezi Januari 2019 watakuwa wamekamilisha zoezi la ujenzi wa Shule mpya ya UTAYARI inayojengwa Kijijini humo.
Hayo yalisemwa na Viongozi wa Kijiji cha Buanga kwa niaba ya Wananchi wao jana tarehe 17. 10. 2018 wakati wakiendelea na zoezi la ufyatuaji wa matofali kwenye eneo la ujenzi wa Shule ya UTAYARI Mpya Buanga.
Awali, akizungumza na Mwandishi wa Habari hizi, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Buanga Ndugu Kejile M. Eyembe alisema, “tunashukuru sana kwa mchango wa Mbunge wa jumla ya Saruji Mifuko 100. Tayari ametupatia Saruji Mifuko 50 leo itakamilika katika hatua ya ufyatuaji wa matofali na kesho tutakabidhiwa  Saruji Mifuko 50 iliyobakia kama alivyoahidi Mbunge alipoendesha Harambee ya ujenzi huu tarehe 9.10.2018. Ujenzi wa boma utaenda kwa kasi kubwa sana.”
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Rusoli Mhe Boazi M. Nyeula amezidi kumshukuru Mbunge kwa dhamira yake ya kujitolea katika kufanikisha Maendeleo Vijijini mwetu.
Mhe Diwani Boazi ameongezea kuwa ana imani na kasi ya Wananchi wa Buanga kwani muda mwingi wapo kazini na kusema, “sisi kama viongozi tutaendelea kuwashirikisha kwa karibu sana Wazawa wa Kata yetu na Kijiji chetu kufanikisha ujenzi huu kabla ya Februari 2019.”
NJOONI TUCHANGIE MAENDELEO KWA VITENDO