KILIMO CHA MAZAO MAPYA YA ALIZETI NA UFUTA CHAFUFUA MATUMAINI YA UCHUMI IMARA JIMBONI

Kilimo cha ALIZETI na UFUTA ndani ya Jimbo la Musoma Vijijini kimefufua matumaini ya kuinua uchumi wa wananchi, shule kadhaa   na vikundi vya maendeleo.
Kwa misimu mitatu mfululizo, mbegu za ALIZETI zimegawiwa bure na Mbunge wa Jimbo wakati mbegu za UFUTA ziligawiwa bure na Halmashauri ya Musoma.
Mkuu wa Wilaya na Afisa Kilimo wa Halmashauri, wamesimamia ugawaji wa mbegu zote na utoaji elimu kuhusu kilimo cha ALIZETI na UFUTA ndani ya Jimbo la Musoma Vijijini.
Awali, akizungumza na Msaidizi wa Mbunge, Mwalimu wa Somo la Kilimo katika Shule ya Msingi Mkirira A, Neema Manyama amesema, “ALIZETI ni zao pekee ambalo tangu lilimwe kijijini hapo limekuwa likistawi na kutoa uhakika wa mavuno mazuri. Hivyo ni vyema jamii zikachangamkia zao hili, ikiwezekana lilimwe na kila kaya kwa ajili ya uhakika wa kipato kizuri.”
 Mwalimu Manyama ameongezea kuwa, Kilimo cha ALIZETI na UFUTA ndio mradi mkuu na wa uhakika shuleni hapo ambapo zaidi ya ekari 2 kwa kila zao zimelimwa na wana matarajio ya kuvuna kwa wingi zaidi huku akizidi kumpongeza Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Prof Muhongo kwa kuwathamini na kuwajali wananchi wa Jimbo lake kwa kubuni kilimo bora na chenye manufaa.
Kwa upande wa Shule ya Msingi Busekera, ambayo  ni msimu wa kwanza kwao kulima ALIZETI wamesema, ALIZETI ni zao pekee lililostawi bila tatizo lo lote na tayari limefikia hatua nzuri. Hayo yalielezwa na  Mwalimu Paschal Abel wa shule hiyo.
Ndugu Godilisten Kenny wa Kijiji cha Saragana, amekiri kwamba kilimo cha ALIZETI kitaongeza kipato cha wakulima ndani ya Jimbo la Musoma Vijijini.
Mazao ya biashara ya Jimbo la Musoma ni: (i) pamba, (ii) alizeti,  na (iii) ufuta. Mihogo na mahindi yatalimwa kwa wingi kwa ajili ya chakula na biashara.